Jeshi la Polisi Mkoa
wa Mwanza limeutaka umoja wa waendesha Bajaji za mizigo (GUTA) mkoani humo,
kutunza amani kwa kutafuta njia sahihi ya kutatua changamoto wanazokutana nazo
katika kazi yao.
Kauli hiyo imetolewa
na kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod
Mutafugwa wakati akizungumza na madereva
hao kwa lengo la kusikiliza na kujadili matatizo waliyonayo ili kuangalia namna
ya kupata ufumbuzi.
Katika mkutano huo,
Kamanda Mutafugwa amewapongeza madereva hao kwa mshikamano wao na ushirikiano
na Jeshi la Polisi katika kutanzua na kudhibiti uhalifu na kuwataka kuzingatia sheria za usalama
barabarani, hasa kuheshimu misafara ya viongozi, magari ya dharura na watumiaji
wengine wa barabara.
Kikao hicho
kimetokana na ombi la Umoja wa waendesha Bajaji kuandika barua ya tarehe
03.06.2025 kwa kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza kuomba kufanya maandamano ya
amani tarehe 13 Juni,2025 bila kuweka wazi lengo na dhumuni la maandamano hayo
ambapo leo wamemueleza Kamanda kuwa wamepandishiwa kodi.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa umoja wa madereva wa Bajaji Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Jeremiah,
alisema wamepokea ushauri wa Kamanda na watawasilisha barua rasmi kwa Serikali
ili kuomba mazungumzo ya marekebisho ya kodi.
"Ulipaji wa kodi
ni uzalendo. Tutalipa kodi zote stahiki ikiwa ni pamoja na za maegesho, vibali
vya RATRA, bima na zingine halali ili kujenga taifa letu,"
alisema Jeremiah.
0 Maoni