Madaktari wa Hospitali ya Benjamin Mkapa wapelekwa Japan kwa mafunzo

 

Timu ya Madaktari, Wauguzi na Wataalamu Mitambo wa Hospitali ya Benjamin Mkapa wako Tokyo nchini Japan kwa mafunzo maalum ya kuzibua mishipa ya kwenye ubongo na kutanua mishipa ya kwenye ubongo bila kufungua fuvu la kichwa.

Mafunzo hayo yanafanyika katika maabara maalumu ya angiosuit Kamagaya General Hospital na Dokkyo University Hospital za Tokyo nchini Japan.

Kiongozi wa Timu kutoka BMH  ambaye ni Mkurugenzi wa Upasuaji wa BMH Dkt. Henry Humba amesema kuwa wamepata nafasi ya kujifunza kuzibua mishipa ya damu ya kwenye ubongo “ thrombectomy” na pia kutanua mishipa ya damu ya kwenye ubongo kwa kuweka stenti “ carrotid stenting”, pia kuzuia sehemu za mishipa ya damu zilizovimba/ kupasuka (aneurysms) na kuziba mishipa ya damu inayoenda kwenye Vimbe za kwenye ubongo ( brain tumor embolization).

"Hii ni maandalizi kwa ajili ya kutoa huduma hii hapo BMH na pia huduma hii ni kipaumbele cha wizara ya afya kwa mwaka ujao wa fedha na fursa hii ya mafunzo yanayotarajiwa kukamilika baadae mwezi Juni, imepatikana kutokana na mashirikiano kati ya BMH na Tokushukai Medical Group ya nchini Japan,” alimalizia Dkt. Humba.

Nae Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya fahamu  Hospital ya chuo Kikuu cha Dokkyo iliyopo Tokyo nchini Japan  Prof. Kensuke Suzuki amesema kuwa  tangu mwezi Mei mwishoni wamekuwa na timu ya wataalamu wa mishipa ya fahamu kutoka BMH Tanzania imekuwa ikitembelea idara yao na kufanya mafunzo, kwa kipindi chote hicho wamepata fursa ya kubadilishana utaalamu na uzoefu.

Chapisha Maoni

0 Maoni