Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amevitaka vyombo vya habari vinavyomilikiwa na chama hicho kuzingatia weledi, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Balozi Nchimbi
amesema vyombo hivyo vina wajibu mkubwa wa kutumia weledi huo kutangaza
mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza Alhamisi,
tarehe 5 Juni 2025, wakati wa kikao na baadhi ya wakuu wa idara wa vyombo vya
habari vya CCM, wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Uhuru Media
Group (UMG), Dennis Msacky, Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa weledi wa vyombo
hivyo uendelee kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya habari nchini.
Mazungumzo hayo
yalifanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es
Salaam, ambapo pia aliwapongeza kwa namna wanavyoendelea kuwahabarisha wananchi
kuhusu masuala yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Balozi Nchimbi
alisema vyombo hivyo vya habari, ambavyo ni sauti ya chama, vina jukumu la
kuutangazia umma utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati chini ya Ilani
ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020–2025, sambamba na kuanza kuchambua Ilani mpya
ya chama hicho kwa mwaka 2025–2030.
Kwa upande wao,
wawakilishi wa vyombo hivyo walieleza namna walivyojipanga kufikisha taarifa
kwa jamii, zikiwemo elimu ya uraia kuelekea uchaguzi, namna ya kushiriki, na
mchakato wa kuwapata wagombea bora ndani ya CCM, kwa lengo la kuhakikisha chama
hicho kinapata ushindi wa kishindo.
0 Maoni