Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa kwa wadau
wote wa mazingira kuendeleza mambo yote yaliyofanyika katika maadhimisho ya
mazingira ikiwa ni pamoja na upandaji miti na uanzishwaji wa bustani za kijani.
Makamu wa Rais ametoa
wito huo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani iliyofanyika
Kitaifa katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Mkoani Dodoma na kuwahimiza wadau hao uhamasisha matumizi ya
teknolojia za urejelezaji wa taka ozo na za plastiki, kupunguza ukataji miti
holela kwa ajili ya kuni na mkaa na kuongeza matumizi ya nishati safi ya
kupikia.
Aidha, Makamu wa Rais
amesema Serikali imeweka nia ya kupunguza athari za uharibifu wa mazingira kwa
kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa shughuli za kupikia. Amesema
katika kutekeleza nia hiyo, Serikali ilitoa katazo la matumizi ya kuni na mkaa
kwa taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya watu mia moja kwa siku
na kuzitaka zihamie katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo kufikia
Machi 2025 jumla ya taasisi 762 zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia kati
ya hizo taasisi za umma ni 495 na taasisi binafsi ni 267.
Halikadhalika Makamu
wa Rais amesema jukumu la kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa
hifadhi ya mazingira linahitaji ushirikiano wa wadau wote katika ngazi zote.
ametoa wito kwa vyombo vya habari, taasisi zote za Serikali, binafsi na asasi
za kiraia kushirikiana katika kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza uharibifu wa
mazingira hapa nchini kwa kiasi kikubwa.
Makamu wa Rais
amesema taarifa mbalimbali za hali ya mazingira nchini zimedhihirisha kuwepo
kwa uharibifu wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo inakadiriwa kuwa
takriban asilimia 61 ya ardhi nchini iko katika hatari ya kuharibika. Amesema
uharibifu huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu zisizo
endelevu, idadi kubwa ya mifugo isiyolingana na uwezo wa malisho, ukataji wa
misitu kwa ajili ya kuni na mkaa, uanzishaji wa mashamba mapya unaotokana na
kilimo cha kuhamahama, uchimbaji holela wa madini pamoja na upanuzi wa makazi
usiozingatia mipango miji.
Makamu wa Rais
amesema katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, Serikali imechukua hatua
mbalimbali za kisera na kimkakati ikiwa ni pamoja na kupitishwa kwa Sera ya
Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi na umilikishaji
wa ardhi kimila.
Amesema hatua
nyingine ni pamoja na uhamasishaji wa matumizi endelevu ya ardhi hususan kilimo
mseto, kilimo cha matuta, kilimo hifadhi na mbinu endelevu za kiasili za
hifadhi ya malisho. na utekelezaji wa hatua hizi ikiwa ni pamoja na kuendelea
kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa ujumla.



0 Maoni