Mkoa wa Dodoma
unajiandaa kuandika historia mpya katika sekta ya usafishaji wa madini,
kufuatia hatua za mwisho za ujenzi wa kiwanda kipya cha Shengde Precious Metal
Resources Company Ltd, kilichopo eneo la Nala, ambacho kinatarajiwa kuanza
rasmi uzalishaji wa copper cathode mwezi Julai, 2025.
Katika ziara maalum
ya ukaguzi, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Menard Msengi,
amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni hatua kubwa kuelekea utekelezaji wa agizo la
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, la kuhakikisha kuwa hadi kufikia
Julai 30, 2025, usafishaji wa shaba yote inayochimbwa nchini unafanyika ndani
ya mipaka ya Tanzania.
“Ujio wa kiwanda hiki
ni kichocheo muhimu katika maendeleo ya Sekta ya Madini mkoani Dodoma na nchini
kwa ujumla,” amesema Mhandisi Msengi, na kuongeza kuwa, “mradi huu
utawanufaisha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia soko la uhakika, kuongeza thamani
ya madini na kuongeza mapato ya wananchi pamoja na taifa.”
Kiwanda hicho ni
miongoni mwa miradi inayofuatiliwa kupitia mradi wa Shirika la Maendeleo la
Umoja wa Mataifa (UNDP), unaolenga kuchochea maendeleo ya Sekta ya Madini ya
viwandani, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa masuala ya mirabaha, usalama
migodini na mchango wa sekta hiyo katika maendeleo endelevu.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa kiwanda cha Shengde, Abia Mafie, amesema tayari kiwanda kimeanza
majaribio ya uzalishaji na kinaweza kuzalisha tani 20 za copper cathode kwa
siku.
“Tunatarajia kuwasili
kwa mitambo mikubwa zaidi itakayoongeza uwezo wetu hadi kuzalisha tani 1,000
kwa siku. Hii itawasaidia wachimbaji wadogo wenye changamoto ya kukosa soko kwa
sababu ya viwango vya kimataifa,” ameeleza Mafie.
Akiwaonesha wageni
jinsi uzalishaji unavyofanyika, Mafie amebainisha kuwa kiwanda hicho kinatumia
kila kipande cha madini kilichopo: “Hata vumbi la copper tunalitumia
kutengeneza tofali – hakuna kinachoachwa.”
Aidha, ametangaza
mpango wa kampuni hiyo kujenga viwanda vingine vitano katika mikoa mbalimbali
ya Tanzania kama sehemu ya mchango wao katika jitihada za Serikali za kuongeza
thamani ya madini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.




0 Maoni