Balozi wa Tanzania
nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amewasilisha rasmi Hati za Utambulisho kwa
Mfalme Carl XVI Gustaf, katika hafla maalum iliyofanyika tarehe 12 Juni, 2025,
katika Kasri la Mfalme wa Sweden, jijini Stockholm.
Baada ya mazungumzo
mafupi kwenye Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufalme wa Uswidi, Mhe. Balozi Matinyi
alisindikizwa kwa gwaride rasmi kuelekea kwenye Kasri la Kifalme na kuwasilisha
hati hizo kwa Mfalme Carl XVI Gustaf, ikiwa ni ishara rasmi ya kuanza kazi yake
kama mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden.
Katika mazungumzo yao
mafupi, Mhe. Balozi Matinyi alimfikishia Mfalme Carl XVI Gustaf salamu za
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwake
yeye binafsi pamoja na serikali na watu wa Uswidi.
Mhe. Balozi Matinyi
alimwelezea pia Mfalme Carl XVI Gustaf dhamira ya Tanzania ya kuendeleza na
kuimarisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizi mbili na
nia ya kukuza ushirikiano katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, hususani
katika uwekezaji, biashara, utalii, elimu na mafunzo ya ufundi, afya, nishati,
miundombinu, utunzaji mazingira, pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi.
Kwa upande wake,
Mfalme Carl XVI Gustaf alituma salamu za undugu na urafiki kwa Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan; na kueleza kuwa nchi
yake ya Uswidi itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa manufaa ya mataifa yote
mawili, hususani katika kuendeleza sekta za viwanda, nishati, madini, utalii na
elimu.
Itakumbukwa kuwa,
Mhe. Matinyi aliteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kuwa Balozi wa Tanzania
nchini Uswidi mnamo tarehe 25 Machi 2025, ambapo pia atakuwa na jukumu la
kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Denmark, Finland, Iceland, Norway,
Estonia, Latvia, Lithuania na Ukraine.
0 Maoni