Tanzania imefanikiwa kutinga katika nafasi ya kumi bora katika mataifa yenye akiba kubwa ya dhahabu Afrika na kuipiku nchi ya Msumbiji iliyokuwa ikishikilia nafasi ya kumi barani Afrika kwa kuwa na hifadhi kubwa ya dhahabu kwenye Benki Kuu.
Mafanikio hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde katika mkutano wake na waandishi wa habari ulioratibiwa na Idara ya Habari-MAELEZO, maalum kwa ajili ya kuelezea mafanikio ya Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Baada ya kufanyika marekebisho ya sheria, BoT ilianza kununua dhahabu… katika takwimu za bara la Afrika nchi inayoongoza kwa kuwa na hifadhi kubwa ya dhahabu ni Algeria kupitia Benki Kuu wana tani 174, wakumi kwenye orodha ni Msumbiji wana tani 3.6 kupitia Benki Juu,” alisema Mhe. Mavunde na kuongeza,
“Sisi Tanzania tumeanza kununua dhahabu kupitia Benki Kuu tarehe 01/10/2024 ninavyosimama leo hii kuzungumza nanyi BoT imeshanunua dhahabu tani 3.7, hivyo moja kwa moja Tanzania imeshaipiku Msumbiji iliyokuwa nafasi ya 10, na huu ndio mwanza wa miezi nane tu,” alisema Mhe. Mavunde.
Kuhusu kuwawezesha Watanzania kushiriki katika sekta ya madini, Mhe. Mavunde amesema ameunda kamati ya watu sita ambayo inayohusisha wataalam wa wizara na sekta binafsi, wataalamu wa masuala ya fedha akiwamo Mkurugenzi Mkuu wa Benki NBC.
“Kamati hii inakuja kuishauri Serikali namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kimitaji na kuwaendeleza, kwa sababu ndugu waandishi wa habari nataka kukiri na kusema hapa hatuwezi kuendeleza uchumi wa madini kama hatutawashika mkono Watanzania,” alisema Mhe. Mavunde.
Kwa upande wa programu ya kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki katika sekta ya madini, Mhe. Mavunde amesema wanaendelea kutoa leseni kwa vikundi vya vijana, ambapo hivi karibuni tarehe 03/05/2025 alikuwa Nyamongo wilayani Tarime na alitoa leseni kwa vikundi 46 vyenye vijana zaidi ya 2000.
“Vijana hao ni wanaozunguka kwenye mgodi wa Nyamongo, na ndio tuliowangiza kwenye programu hii kwa awamu ya kwanza, na bahati nzuri tumepata muitikio wa wenzetu wa Benki ya Dunia, wameiona ni programu ambayo wanaweza kuiunga mkono na hivi sasa tupo katika mazungumzo,” alisema Mhe. Mavunde.
Ameeleza kuwa Wizara yake wiki hii inategemea kumpokea ugeni kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya majadiliano ya programu hiyo, lakini pia baraza la dhahabu la dunia (World Gold Council) wameonyesha nia ya kuunga mkono programu hiyo.



0 Maoni