Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amekitaka Chama Chama cha Watoa Huduma Sekta ya Madini (TAMISA), kujiandaa kikamilifu kukabiliana na upinzani kutoka kwa wageni katika kunufaika na fedha shilingi trilioni 3.1 zinazotumika kila mwaka na migodi mikubwa ya madini kwa ajili ya manunuzi.
Mhandisi Samamba ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam, wakati akizindua Kamati ya Chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), pamoja na Kongamano la Kuwaunganisha Watanzania waliopo katika sekta ya madini.
“Tunaenda kuingia kwenye vita, hii ni vita ya kiuchumi, unapoingia ndani unamkuta mtu anakula na wanawe pilau halafu wewe ukalipiga bakuli teke, unategemea nini?, unatarajia nini?, ukinzani utakuwepo na ni hulka ya binadamu ukimfanyia mabadiliko atakaidi ni kawaida,” alisema Mhandisi Samamba na kuongeza,
“Kwa sasa usambazaji umekuwa ukifanywa na watu kutoka nje, hizi shilingi trilioni 3.1 tulizosema zinachukuliwa na watu kutoka nje, tunakwenda kubadilisha upepo kupitia TAMISA, kwahiyo muwe tayari kwa changamoto sio changamoto zinakuwa kubwa mnasema hii ishakuwa shida, mnabonyea, mkibonyea hamtafanikiwa.”
Amsema kwamba Serikali imebadilisha sheria na imebadilisha kanuni, hivyo basi anawataka TAMISA kuishauri Serikali kama kuna upenyo wa kisheria ama kanuni unaotumika kuwaminya Watanzania Watoa Huduma Sekta ya Madini, hali hiyo idhibitiwe.
“Tunataka waje watu washirikiane na watu wanaofanya shughuli za utoaji huduma kwenye migodi Watanzania, kwasababu kifungu cha sheria ya madini namba 102 kipo wazi katika hilo kwamba kazi zote za madini zitatolewa kwa Watanzania, isipokuwa pale tu hakuna Mtanzania mwenye uwezo ndipo utaundwa ushirikiano kati ya Watanzania na wageni,” alisema Mhandisi Samamba.
TAMISA iliyozinduliwa Septemba 15, 2024 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, inamalengo makuu ya kutetea wasambazaji wa sekta ya madini, kuboresha uwezeshaji wa biashara, kutetea haki za wasambazaji na kuendeleza utafiti na ukuaji wa teknolojia.

0 Maoni