Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj
Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza Waislamu, wahisani na wafadhili
kuelekeza nguvu zao katika kuziimarisha Madrassa, kwani nyingi bado ziko katika
mazingira yasiyoridhisha, pamoja na kuwasaidia Masheikh na Walimu wa Madrassa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Msikiti wa
Jibril uliopo Fuoni Bwiti, Mkoa wa Mjini Magharibi, tarehe 16 Mei 2025.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Serikali inafarijika
inapowaona wadau na wafadhili mbalimbali wakijitokeza kusaidia huduma za
kijamii katika sekta mbalimbali, kwani hatua hiyo husaidia kupunguza mzigo kwa
Serikali.
Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wana-Diaspora, hususan vijana
wenye ujuzi katika ujenzi wa skuli, hospitali, huduma za afya na sekta nyingine
za kijamii, kurejea nyumbani na kuungana na Serikali kuleta maendeleo ya taifa.
Akizungumzia Msikiti alioufunguwa, amewahimiza Waislamu
kuutunza na kuutumia kwa ibada kwa bidii ili dhamira ya wafadhili waliochangia
ujenzi wa msikiti huo itimie.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amezipongeza Taasisi za
Tears of Joy na Jibril Foundation kwa usimamizi mzuri uliofanikisha ujenzi wa
msikiti huo.
Kuhusu suala la amani, Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa
Wazanzibari kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu ili nchi iendelee kupiga
hatua zaidi za maendeleo.
Ameeleza kuwa mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yametokana na kuwepo kwa amani, jambo linalopaswa kuendelezwa kwani Serikali imejipanga kufanya mambo makubwa zaidi katika miaka mitano ijayo.




0 Maoni