WAZIRI wa Madini Mhe. Anthony Mavunde aliweka wazi mafanikio 16 ya Sekta ya Madini katika kipindi cha Miaka Minne ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania kununua Tani 3.7 kwa gharama ya Shilingi 702.3 Bilioni.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Mei 15, 2025, katika ukumbi wa Idara ya
habari (MAELEZO), Waziri Mavunde alisema kati ya kiasi kilichonunuliwa
takribani, Kilo 2,954 zilisafishwa katika viwanda vya kusafisha dhahabu
vilivyoko nchini.
Mhe. Mavunde alisema katika Bara la Afrika nchi tano
zinazofanya vizuri katika ununuzi wa dhahabu, Tanzania ipo huku nchi ya Algeria
ikiongoza.
“Miaka mingi nchi yetu iliacha kununua dhahabu kupitia Benki
Kuu, lakini mwaka wa fedha 2024/2025 tulifanya marekebisho ya Sheria ya Madini
kifungu cha 59 sura ya 123 ambacho kinampa dhamana Waziri wa Madini kujadiliana
na wamiliki wa leseni kutenga asilimia 20 ya madini yanayozalishwa na
kuchakatwa ndani ya nchi kuyeyushwa na kusafishwa kununuliwa na BOT ili kukuza
hifadhi ya fedha za kigeni kupitia ‘monetary gold’ ambayo ina manufaa makubwa
kwa ukuaji na ustahimilivu wa Uchumi wa Taifa,” amesema Waziri Mavunde na
kusisitiza:
“Nchi inayoongoza Afrika kwa kuwa na hifadhi kubwa ya
dhahabu ni Algeria, katika kumi bora kwenye orodha ilikuwa ni Msumbiji wana tani
3.6, sisi Tanzania tumeanza kununua dhahabu Oktoba 1, 2024 mpaka sasa Tani 3.7
tumeshampiku aliyekuwa kumi bora na huu ndio mwanzo ni miezi nane tu, miaka
mitano ijayo tutakuwa mbali,” amesema.
Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza rasmi ununuzi
wa dhahabu Oktoba 1, 2024, kupitia viwanda vitatu vya kusafisha dhahabu vya
MPMR (Mwanza), GGR (Geita), na Eyes of Africa (Dodoma).
Aidha, alisema mkakati wa Wizara ya Madini ni kuhakikisha
Serikali kupitia Benki Kuu, inaangalia uwezekano wa kuanzisha uuzaji wa sarafu
za dhahabu zenye uzito ili kuwaongezea watanzania wigo wa uwekaji akiba na
uwekezaji kupitia ununuzi wa dhahabu.
“Vilevile hatua hii itaongeza umiliki wa dhahabu miongoni
mwa wananchi, kuimarisha soko la ndani la dhahabu, na kuimarisha mzunguko wa
fedha ndani ya nchi,” alisema Mhe. Mavunde.
Uongezaji Thamani Madini
Waziri Mavunde alisema tayari kuna jumla ya viwanda 8 vya
kusafisha dhahabu nchini na hivi sasa Serikali inavisaidia kuweza kukidhi
viwango vya kimataifa na kuongeza kwamba, tayari Serikali imetenga eneo maalum
la uwekezaji kwa ajili ya viwanda vya uongezaji thamani madini na bidhaa
zinazotumika migodini la Buzwagi Special Economic Zone mahali ulipokuwa mgodi
mkubwa wa uchimbaji dhahabu Buzwagi na kueleza kwamba, hadi sasa tayari viwanda
kadhaa vimeanza kazi ikiwemo cha kutengeneza vipuri cha East African Conveyor
Supplies Limited (EACS), huku kiwanda cha kusafisha madini ya metali cha
kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited.
Ununuzi wa Mafuta na Fedha za Kigeni kutumia Dhahabu
Waziri Mavunde alisema pia, Serikali kupitia Benki Kuu, itafikiria kuanzisha utaratibu wa kutumia dhahabu itakayonunuliwa, hususan isiyokidhi vigezo vya kuingia katika soko la LBMA, kubadilishana na nishati ya mafuta (barter trade) na kununulia fedha za kigeni kulingana na mahitaji ya nchi.
Ununuzi wa Fedha za Kigeni zinazotokana na Mauzo ya Madini
Waziri Mavunde alisema sheria inayotaka kampuni na
wafanyabiashara kurejesha fedha zinazotokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi,
ikiwemo madini, itaendelea kusimamiwa ipasavyo.
“Iwapo Serikali itaipa Benki Kuu ya Tanzania haki ya kwanza (Pre-emption right) ya kununua fedha hizo zinazorejeshwa nchini na kuwalipa wahusika kwa Shilingi ya Tanzania itasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni na kuimarisha umadhubuti wa shilingi na viwango vya ubadilishaji fedha,” alisema Waziri Mavunde.
#InvestInTanzaniaMiningSector
#Mining4Development
#Vision2030: MadininiMaishanaUtajiri


0 Maoni