Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka viongozi wa Mitaa
na Vijiji pamoja na wananchi kwa ujumla katika mikoa 16 inayoendelea na zoezi
la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kushirikiana na watendaji wa
zoezi hilo vituoni kutoa taarifa za Wapiga Kura waliopoteza sifa za kuwepo
katuika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akiwa Wilayani Mafia, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, alishuhudia wenye viti wa
Mitaa katika vituo mbalimbali alivyopita wakiwaondoa katika Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura katika zoezi linaloendelea la Uboreshaji wa Daftari awamu ya pili.
Akizungumza baada ya kutembelea Vituo vya Uboreshaji
Wilayani humo, Jaji Mwambegele aliwa pongeza viongozi wa serikali za mitaa
katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani wanavyoshiriki katikia
uhakiki wa Daftari la awali la Wapiga Kura na kubaini watu ambao wamepotesa
sifa hivyo kuwatolea taarifa na kuondolewa katika Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura.
“Viongozi wa hapa Mafia wamejitokeza vizuri kuja na orodha
ya watu wasiostahili tena kuwepo kwenye Daftari, sasa nawasihi viongozi katika
mikoa hii 16 hapa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar pale ambapo wanaona kuna
mwenyeji wao amepoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
basi wasisite kuja kujitokeza na kufuta taarifa zao,”alisema Jaji Mwambegele.
Aidha, Jaji Mwambegele amesema zoezi la uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa yote 16 limeanza vizuri na vituo
vimefunguliwa kwa wakati na kuwataka wananchi ambao hawakupata fursa ya
kujiandikisha hapo awali basi wafanye hivyo sasa ili wapate fursa ya kushiriki
katika Uchaguzi Mwezi oktoba mwaka huu.
Afisa Mwadikishaji wa Jimbo la Mafia, Mohamed Hussein Othman
akizungumzia zoezi hilo amesema limeanza vyema katika vituo vyote 15 ndani ya
jimbo hilo na wananchi waliokosa fursa ya kujiandikisha na kuboresha taarifa
zao hapo awali wanajitokeza hivi sasa.
“Zoezi letu la Uboreshaji wa daftari la Kudumu la Wapiga
Kura limeanza vizuri, vituo vyote 15 vimefunguliwa saa 2:00 asubuhi wananchi
wanajitokeza kuboresha taarifa zao na wale ambao hawakupata fursa katika
uboreshaji wa awamu ya kwanza nao wanajitokeza kuhakikisha kwamba wanakuwepo
katika Dafrari la Kudumu la Wapiga Kura,”alisema Othman.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Vunja nazi kilichopo Kata ya
Kilindoni Wilayani Mafia, Mwl. Omar Mngwali amesema yeye amekua kiongozi katika
kitongoji hicho kwa muda mrefu na kushiriki vyema katika shughuli za kijamii
imemuwezsha kutambua watu wake waliopoteza sifa wapatao 11 na kutoa taarifa ili
waondolewe kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mzunguko wa pili wa uboreshaji umeanza leo Mei 16 na utaenda
hadi Mei 22, 2025 unahusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga,
Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi,
Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo zoezi
hilo litafanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025.
Zoezi hilo linakwenda sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la awali la Wapiga Kura ambapo wananchi watapata fursa ya kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa na litabandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza.
Vituo vinafunguliwa Saa 2:00 asubuhi na kufungwa Saa 12:00 jioni kila siku kwa siku zote saba za utekelezaji wa zoezi hilo.

0 Maoni