Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA), Mhandisi Victor Seff ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi wa Uboreshaji
wa Miundombinu ya Miji Tanzania kwa Awamu ya Pili (TACTIC) jijini Arusha
kutabadilisha muonekano na mandhari ya jiji hilo kuendana na hadhi yake ya mkoa
wa kitalii, kuongeza fursa za ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha
hali ya biashara na hivyo pia kuchangia maendeleo ya kijamii.
Mhandisi Seff amebainisha hayo hivi karibuni jijini Arusha
wakati wa utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo utakaohusisha
ujenzi wa kituo kikuu cha Mabasi Bondeni city, Ujenzi soko kuu la Kilombero,
Ujenzi soko la Morombo pamoja na uboreshaji wa bustani ya mapumziko ya Themi
Living Garden, miradi itakayotekelezwa na mkandaradi M/s Mohammed Builders
Limited kwa gharama ya 30,625,112,436.85 bila ya VAT.
Kulingana na Mhandisi Seff kukamilika kwa Kituo kikuu cha
Mabasi Jiji la Arusha kutawezesha uwepo wa vibanda vya wafanyabiashara 900
kutoka 250 vya sasa, mifumo ya ulinzi kwa kutumia Camera za CCTV, maegesho ya
magari pamoja na huduma nyinginezo, zitakazowezesha makusanyo kuongezeka kutoka
Milioni 72 kwa Mwezi hadi Shilingi Milioni 260.
Aidha, kukamilika kwa ujenzi wa Soko la Kilombero, mbali ya
kubadilisha muonekano wa Jiji la Arusha, soko hilo litakuwa na Vibanda 3,274
kwaajili ya wafanyabiashara na wajasiriamali pamoja na huduma nyinginezo za
ulinzi kwa kutumia kamera za CCTV, huku soko La Morombo likiwekwa Vibanda 752
kutoka vibanda 587 vya sasa na hivyo kuchangia kwenye makusanyako ya Jiji
kufikia jumla ya Milioni 117 kwa mwezi kwa masoko yote mawili.
Kuhusu Bustani ya Themi, Mhandisi Seff ameeleza kuwa eneo hilo litakuwa na maeneo rasmi ya kupumzikia kwa faragha mbalimbali, mfumo rasmi wa uendeshaji, huduma za vyakula, viburudisho na burudani. Maegesho mbalimbali, vyoo na huduma za kujisitiri kwa wanawake, bustani za miti na maua pamoja na ulinzi wa kamera za CCTV.



0 Maoni