Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan, amepongezwa kwa maono yake ya mbali na uamuzi wa busara wa
kumpendekeza Profesa Mohamed Yakub Janabi kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa
Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Wananchi mbalimbali waliohojiwa wametaja hatua hiyo ya Rais
Samia kama ishara ya kujiamini kama taifa, na uthibitisho kuwa Watanzania wanao
uwezo wa kushika nafasi nyeti katika taasisi kubwa za kimataifa, wakielezea
faraja yao kwa jinsi Tanzania inavyozidi kung’ara kwenye majukwaa ya
kidiplomasia duniani.
Aidha, Rais Samia amesifiwa kwa kuunda kikosi kazi maalum
kilichoongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, kwa ajili ya kuratibu na kusimamia kampeni ya kidiplomasia ya Profesa
Janabi.
Ushirikiano huo umeibuka na
matokeo chanya, ambapo Profesa Janabi ameibuka mshindi kwa kishindo
kupitia mchakato wa uchaguzi uliopigiwa kura na nchi wanachama wa WHO Kanda ya
Afrika.
Dkt. Kikwete, ambaye ana uzoefu mkubwa katika medani za
kimataifa, amepongezwa kwa kutumia umahiri na uhusiano wake wa kidiplomasia
kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa. Mchango wake umetajwa kama kichocheo
muhimu kilichowezesha Tanzania kupata ushindi dhidi ya wagombea kutoka Côte
d’Ivoire, Guinea na Togo.
Katika picha iliyopigwa wakati wa harakati za kampeni hiyo,
Dkt. Kikwete anaonekana akiongoza moja ya vikao vya kikosi kazi hicho, ambacho
hatimaye kilitimiza azma yake mnamo Jumapili, Mei 18, 2025, kwa ushindi mkubwa
wa Profesa Janabi.
Mgombea huyo wa Tanzania alipata kura 32 kati ya 47
zilizopigwa kwa siri na wajumbe wa nchi wanachama wa WHO Afrika, kabla ya
kuanza kwa Mkutano Mkuu wa WHO.
Uchaguzi huo umefanyika kufuatia kifo cha ghafla cha
aliyekuwa Mkurugenzi mteule, Dkt. Faustine Ndugulile, mnamo Novemba 2024. Nafasi
hiyo ilivuta wagombea mahiri kutoka mataifa kadhaa, lakini Profesa Janabi
alifanikiwa kuungwa mkono kwa wingi, akionesha kuwa jina la Tanzania bado lina
nguvu katika diplomasia ya afya barani Afrika.
Kwa mujibu wa taratibu za Shirika la Afya Duniani, jina la
Profesa Janabi sasa litawasilishwa kwa ajili ya kuthibitishwa rasmi na Bodi ya
Utendaji ya WHO katika kikao chake cha 157 kitakachofanyika Mei 28–29, 2025,
mjini Geneva, Uswisi.
Iwapo atathibitishwa, Profesa Janabi ataapishwa na kuanza kutekeleza rasmi majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitano, huku akiwa na fursa ya kuongezewa muhula mmoja zaidi kulingana na kanuni za taasisi hiyo.
0 Maoni