Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ushirikiano na mshikamano ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mikoa yao.
Akizungumza leo Mei 20, 2025, katika mafunzo ya uongozi kwa
Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi mkoani
Pwani, Msovela amesema kuwa ushirikiano ni nguzo muhimu katika kufanikisha
malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka
na yenye tija.
“Ni muhimu tufanye kazi kama timu moja. Miradi ya maendeleo
haiwezi kutekelezwa kwa ufanisi ikiwa kila mmoja atafanya kazi kivyake.
Ushirikiano, mawasiliano na uwajibikaji ni mambo ya msingi,” amesisitiza
Msovela.
Aidha, ameongeza kuwa Makatibu Tawala Wasaidizi wanapaswa
kuratibu kwa ufanisi shughuli zote za maendeleo, kufuatilia utekelezaji wake
kwa karibu na kutoa taarifa sahihi kwa wakati ili kuisaidia Serikali kufanya
maamuzi yenye tija.
Msovela amesema viongozi hao ni kiungo muhimu kati ya
wananchi na Serikali, hivyo ni lazima wawe karibu na wananchi, kusikiliza
changamoto zao na kushirikiana nao katika kuzitafutia
suluhisho la kudumu.



0 Maoni