WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya
Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti
katika kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi zikiwemo za
sekta ya elimu.
Ameyasema hayo jana (Jumatatu, Mei 19, 2025) wakati
akizungumza na wananchi katika mikutano wa hadhara iliofanyika Sengerema mjini
na Buchosa wilaya ya Sengerema akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri Mkuu amesema miongoni mwa hatua ambazo Serikali
imezichukua ni pamoja na kuendelea kutoa elimu msingi bila ya ada na hivyo
kuwawezesha watoto wa kitanzania wenye umri wa kwenda shule kupata elimu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa sasa Serikali inaendelea na
ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali nchini hususani
katika yale yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi.
”Mkakati mwingine mkubwa unaoendelea kutekelezwa na Serikali
ni ujenzi wa mabweni, nyumba za walimu, pamoja na kujenga shule za amali ili
wanafunzi watakapomaliza shule hizi waondoke na ujuzi.”
Akizungumzia kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya
maji safi na salama, Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikali inatekeleza miradi
ya maji ikiwemo ya kutoa maji katika Ziwa Victoria na kuyasambaza kwa wananchi,
hivyo amewataka waendelee kuwa na subira.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa uongozi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema uhakikishe unakamilisha mchakato wa ujenzi
wa mradi wa soko la halmashauri hiyo ili Sengerema iweze kuwa kituo kikubwa cha
biashara.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewahakikishia wakazi wa wilaya ya Sengerema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kumkabidhi mkandarasi kazi ya ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge ili aanze ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.


0 Maoni