WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka
mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto ya uwepo wa magugumaji katika ziwa
Victoria inapatiwa ufumbuzi ili kuwezesha shughuli za kijamii ziweze kuendelea
katika maeneo hayo.
”Ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuridhia kutoa fedha za ununuzi wa mitambo mikubwa ya kuteketeza magugumaji
ndani ya ziwa Victoria ili kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji
kuendelea.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Mei 19, 2025)
wakati akizungumza na wananchi alipokagua shughuli ya udhibiti wa magugumaji
katika eneo la Kigongo-Busisi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Mheshimiwa Majaliwa amesema magugumaji hayo yamekuwa
yakiathiri kwa kiwango kikubwa shughuli mbalimbali za kijami na kiuchumi katika
ziwa hilo, hivyo ununuzi wa mitambo hiyo utasaidia kuteketezwa kwa magugu hayo.
Aidha, Waziri Mkuu amewashukuru wananchi wa maeneo hayo
wakiwemo wavuvi ambao wamejitolea kushirikiana na Serikali katika zoezi la
kuyaondoa magugumaji hayo.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira iendelee na kazi ya
kuyaondoa magugumaji hayo hadi pale yatakapomalizika ili kuhakikisha shughuli
za kijami zinaendelea bila ya kikwazo chochote.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais
Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa taarifa kuhusu shughuli
ya kuteketeza magugumaji hayo kwa Waziri Mkuu amesema kwa sasa wanaendelea na
kazi ya kuyaondoa magugumaji ya asili ambayo yamesambaa katika eneo la ukubwa
wa ekari zaidi ya 300.
Amesema magugumaji hayo ambayo yamegawanyika katika aina
tatu (salivinia molesta ambalo ni jipya, water hyacinth na gugumaji la asili
aina ya Lutende) yameathiri mfumo wa ikolojia, shughuli za usafiri na
usafirishaji na shughuli za uvuvi katika baadhi ya maeneo ndani ya Ziwa
Victoria.
Katibu Mkuu huyo amesema wanatarajia kumaliza kazi ya kuyateketeza magugumaji mwezi Julai, 2025 na hivyo kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea katika ziwa Victoria kama ilivyokuwa awali.
0 Maoni