Viongozi na wachezaji wa Timu ya Young Africans (Yanga) leo hii wamefanya ziara katika Bustani ya Wanyamapori Hai Tabora, maarufu kama Tabora Zoo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza utalii wa ndani na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. Ziara hii iliongozwa na Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said ikijumuisha wachezaji maarufu wa klabu hiyo.
Katika
mazungumzo yake baada ya ziara, Injinia Hersi Said alisema kuwa lengo kuu la
ziara hiyo ni kuonyesha mchango wa klabu ya Yanga katika kukuza utalii wa ndani
na vilevile kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutangaza vivutio vya utalii vya nchi
yetu.
“Ziara yetu
hapa ni sehemu ya kuonyesha michango yetu katika kukuza utalii wa ndani, ikiwa
ni njia mojawapo ya kuhamasisha Watanzania kutembelea vivutio vyetu vya utalii,
lakini pia kuchangia uchumi wa taifa,” alieleza.
Katika
kutekeleza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza utalii wa ndani, Rais
wa Yanga alitoa wito kwa Watanzania, hasa wakazi wa Mkoa wa Tabora na mikoa
jirani, kutembelea bustani hiyo ya wanyamapori ili kuendelea kuchangia uchumi
wa Taifa kupitia utalii huku akisisitiza kuwa, Yanga, kama klabu kubwa ya soka
nchini, ina nafasi ya pekee katika kutoa mchango mkubwa katika masuala ya
kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha shughuli za utalii.
Hersi pia
alitoa pongezi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa
juhudi zao katika kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya bustani hiyo.
Aliipongeza TAWA kwa kazi nzuri ya kuboresha
mazingira ya hifadhi, akisema, “Pongezi kwa TAWA kwa mapokezi ya kipekee na
huduma bora wanazozitoa. Maendeleo haya ni muhimu katika kukuza utalii wa ndani
na kufanya vivutio vyetu kuwa vya kimataifa.”
Kwa upande
wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi na Kaimu
Kamanda wa Kanda hiyo, Wilbright Munuo, alieleza umuhimu wa Bustani ya
Wanyamapori Hai Tabora katika kukuza utalii wa ndani.
Munuo alisisitiza
kuwa bustani hiyo ina mchango mkubwa katika kuhamasisha jamii kutunza
rasilimali wanyamapori na kulinda mazingira. Alitoa wito kwa Watanzania
kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa wanyamapori na mazingira yao
vinahifadhiwa kwa manufaa ya taifa kwa ujumla. “Tunapaswa kuendelea kutunza
wanyamapori wetu ili vizazi vijavyo vione na kufurahia rasilimali hizi. Hii ni
sehemu ya kutimiza malengo ya kitaifa ya uhifadhi na maendeleo,” alisema.
Wachezaji wa
Yanga pia walionyesha furaha yao kutokana na ziara hiyo na walieleza
kufurahishwa na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika bustani ya
wanyamapori. Wachezaji maarufu kama Pacome, Diarra, Jonas Mkude, na Clement
Mzize walionyesha kuvutiwa na mnyama Simba ambaye ni kivutio kikubwa katika hifadhi
hiyo. Pacome na Diarra walieleza jinsi walivyovutiwa na mandhari ya hifadhi na
wanyamapori waliokuwepo, huku wakiutaja mnyama Simba kama mmoja wa wanyama
waliowavutia zaidi.
Ziara ya timu
ya Yanga katika Bustani ya Wanyamapori Hai Tabora ilifanyika mara baada ya
kumaliza mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Tabora United, ambapo Yanga ilishinda
kwa mabao matatu kwa nunge.
Na. Beatus
Maganja - TABORA




0 Maoni