WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanya maboresho zaidi ya mazingira
ya biashara na uwekezaji ili kuifanya Tanzania iendelee kuwa sehemu salama
zaidi ya uwekezaji.
Mheshimiwa
Majaliwa ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Aprili 3, 2025) wakati wa uzinduzi
wa Maandalizi ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Nchini (MKUMBI II) katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Amesema
kupitia mpango ambao ameuzindua, maandalizi yake pamoja na kamati zake,
Serikali itaweza kushughulikia mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, na kiteknolojia
na kuweka mazingira bora zaidi kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
“Serikali
itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa wadau wote ili kufanikisha malengo ya
kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara. Ni mategemeo yetu kuwa,
mpango huu utaongeza tija kubwa kwa Taifa letu na kusaidia kufikia malengo yetu
ya kuwa na uchumi wa kati ulio endelevu.”
Akizungumza
kuhusu umuhimu wa MKUMBI II, Waziri Mkuu amesema kuwa ni pamoja na kuvutia
wawekezaji wa nje na ndani, kuongeza fursa za ajira, kuboresha miundombinu,
upatikanaji wa soko la kimataifa kwa bidhaa za ndani, kukuza ushindani na ubora
wa bidhaa.
Aidha,
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuisisitiza kamati ya maandalizi ya
MKUMBI II iharakishe maandalizi ya mpango huo ili utekelezaji wake uweze kuanza
mara moja na kurahisisha mazingira bora kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
Pia, Waziri
Mkuu amezitaka Taasisi na Mamlaka za Udhibiti za Serikali ambazo zitahusishwa
katika utafiti na tathmini zitoe ushirikiano wa dhati kwa kamati ili iweze kuja
na mapendekezo mahsusi yenye malengo mapana ya nchi ambayo yataendana na Dira
ya Taifa 2050.
Kwa upande
wake, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo
amesema lengo la Serikali la kuandaa mpango huo ni pamoja na kuona kuwa
Tanzania inakuwa sehemu bora na ya kuvutia ya kufanya biashara na uwekezaji.
“Kazi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ni kazi endelevu.”
Amesema ili
uchumi uweze kukua ni lazima mazingira ya biashara na uwekezaji yafanyiwe
mapitio na maboresho ya mara kwa mara, na ndio maana kamati ya kitaifa ya
wataalam iliyoundwa imezingatia matakwa ya sasa ya uhitaji wa biashara na
uwekezaji.


0 Maoni