MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Joseph Kulangwa, ametoa mwito kwa taasisi za habari kuimarisha ushirikiano na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha upatikanaji wa sheria bora za habari zitakazohakikisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Kulangwa ameyasema hayo jana wakati wa mkutano wa (side event) ulioandaliwa
na TEF, LHRC na MCT katika siku ya ufunguzi ya maadhimisho ya siku ya uhuru
duniani yaliyofanyika mjini Arusha leo.
Katika kuimarisha ushirikishwaji wa wadau, Kulangwa
amezitaka kamati za Bunge kutoa notisi za muda mrefu kwa wadau kabla ya vikao
vya kutoa maoni, ili kuwapa nafasi ya kutosha kujiandaa na kuwasilisha
mapendekezo yao kwa ufanisi.
Kwa upande mwingine, Mhe. Neema Lugangira, Mbunge wa Viti Maalumu kupitia nafasi ya NGOs, amehimiza taasisi za habari kushirikiana na Serikali tangu hatua za awali za mchakato wa marekebisho ya sheria.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wadau kushirikiana na
Serikali kuandaa mapendekezo ya maboresho ya sheria badala ya kuyatayarisha
peke yao na kuyawasilisha mwishoni kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake Dk. Kizito Mhagama amesisitiza umuhimu wa taasisi za habari kuendelea kushauri Bunge kwa kina na weledi, ili kuhakikisha zinapatikana sheria bora zinazokidhi mahitaji ya sekta ya habari na kulinda uhuru wa vyombo vya habari.



0 Maoni