Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa amesema kuwa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
yameiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta mbalimbali
ikiwemo ya Anga.
Amesema hayo jana
Jumatatu (Aprili 28, 2025) wakati alipofungua Mkutano wa 73 wa Baraza la
Kimataifa la Viwanja vya Ndege kwa Ukanda wa Afrika (ACI Afrika) unaofanyika
kwenye Hotel ya Mount Meru.
Amesema kuwa moja ya eneo ambalo Rais Dkt.
Samia ameendelea kusimamia ni ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege nchini
ikiwemo ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha msalato kilichopo jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia anaendelea na
uboreshaji wa viwanja vingine vya kimkakati vya Kilimanjaro, Unguja, Pemba,
Mwanza, Kigoma, Tabora, Shinyanga na Sumbawanga. “Pia tunaendeleza Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Serengeti unaolenga kukuza utalii wa mazingira huku
tukihifadhi mfumo ikolojia wa Serengeti”.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
Serikali imewekeza katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya mawasiliano kwenye
viwanja wa ndege na masafa marefu ili kuhakikisha kunakuwa na usalama wa ndege
na abiria.
Amesema kuwa kutokana na jitihada mbalimbali
za Serikali za kuiimarisha Sekta ya anga, Tanzania imetajwa na Shirika la ICAO
kushika nafasi ya nne barani Afrika kwenye masuala ya usalama wa anga
Kadhalika Uwanja wetu wa ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere umefanikiwa kushinda Tuzo ya Usalama ya Baraza la Viwanja vya
Ndege Duniani, katika viwanja vyenye miruko ya ndege 50000 kwa mwaka”
Akizungumzia kuhusu shirika la ndege la
Tanzania (ATCL) Waziri Mkuu amesema hivi sasa ndege zake zinatoa huduma ya
usafiri katika viwanja 15 vya ndani na nje ya nchi katika nchi za Dubai,
Mumbai, Guangzhou, Johannesburg, Nairobi, Harare, Lusaka, Entebe na Kinshasa
“Shirika pia linatarajia kuongea safari zake
katika miji ya London, Lagos, Accra, Juba, Muscat na maeneo mengine ya masoko
ya kimkakati ili kuiunganisha Tanzania Kikanda na Kimataifa”
Kwa Upande wake, Waziri wa Uchukuzi Profesa
Makame Mbarawa amesema kuwa mkutano huo Inatoa jukwaa adimu linalowaleta pamoja
viongozi na wasimamizi wa usafiri wa anga, waendeshaji wa viwanja vya ndege
kujadili na kubadilishana mawazo katika kuboresha na kuikuza sekta ya usafiri
wa Anga.
Naye Rais wa
Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika Emmanuel Chaves amesema kuwa mafanikio
endelevu sekta ya anga afrika sio tu kwenye utungaji wa Sera bali kwenye
maamuzi tunayoyafanya sasa katika kushirikiana “Kama tutaamua kwa dhati
tutajenga Afrika yenye muunganiko na ushindani
katika sekta ya anga.”
0 Maoni