Serikali imesema itahakikisha inafanyia kazi mapendekezo
yote yatakayotolewa kwenye maazimio ya pamoja ya Waandishi wa Habari baada ya
kuhitimisha Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa
mwaka 2025.
Hakikisho hilo la Serikali limetolewa jana Aprili 28, 2025
na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa
Serikali Bw. Gerson Msigwa wakati akitoa neno la kufunga Siku ya Kwanza ya
Kongamano hilo linalofanyika jijini Arusha kwa uratibu wa Jamii Africa, UNESCO
na Wizara yenyewe.
"Nimesikia maazimio ya awali mliyoyatoa hapa, ni muhimu
sana na mimi nitaomba mkishakamilisha ile nakala ya mwisho mtupatie ili na sisi
serikalini yale ambayo tunatakiwa tuchukue hatua tuyafanyie kazi, basi
tutafanyia kazi mara moja", amesema Msigwa.
Amewapongeza wadau wote walioshiriki Kongamano hilo na kwa
majadiliano waliyoyafanya ikiwemo suala la matumizi ya Akili Mnemba kwa kuwa ni
jambo muhimu kwenye kazi za uandishi wa habari kwa sasa.
Bw. Msigwa amesema Serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa
vyombo vya habari nchini na kwamba hilo linajidhihirisha kwani kumekuwa na
mazingira rafiki kwa Waandishi wa Habari pale wanapotekeleza majukumu yao.
"Sisi Waandishi wa Habari kwenye Awamu hii ya sita
tumekuwa tukifanya kazi katika mazingira rafiki sana, kwa sababu ya maelekezo
ambayo Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) anayasimamia," amesisitiza
Msigwa na kuongeza;
"Aliyoyasema tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani
ndiyo anayoyatekeleza na sisi lazima tutekeleze maelekezo yake kuhakikisha kuna
uhuru wa vyombo vya habari, kuhakikisha waandishi wa Habari hawabughudhiwi
lakini kuendelea kujenga mazingira bora kwa waandishi wa habari kufanya kazi
zao."
Kongamano hilo la Maadhimisho ya Siku ya Siku ya Uhuru wa Habari linatarajiwa kufungwa leo tarehe 29 Aprili, 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
0 Maoni