KATIKA mwaka 2025/26, Serikali imetenga Sh.Bilioni 66.57 kwa
ajili ya kujenga matundu 28,580 ya vyoo
katika shule za msingi na sekondari.
Akijibu hoja ya wabunge kuhusu serikali kufanya tathimini ya
kubaini ubora na ukubwa wa tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo katika shule
zote za msingi na sekondari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed
Mchengerwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa kulinda afya za walimu na
wanafunzi, hivyo itaendelea kukabiliana na changamoto hiyo kwa lengo la kulinda
utu na afya za wanafunzi.
Amesema Sensa ya Elimumusingi ya mwaka 2024 inaonesha
mahitaji ya matundu ya vyoo katika shule za msingi ni 429,599 wakati yaliyopo
ni matundu 240,320, hivyo kuwa na upungufu kuwa ni matundu 189,279, hivyo
kufanya wastani wa uwiano kwa wavulana ni 1:47 badala ya 1:25 unaohitajika na
kwa wasichana kuwa ni 1:43 badala ya 1:20.
Kwa upande wa sekondari, mahitaji ni matundu 135,870 wakati
yaliyopo ni matundu 84,608 na upungufu ni matundu 51,262, hivyo kufanya wastani
wa uwiano uliopo kwa wavulana ni 1:36 badala ya 1:25 na wasichana ni 1:35
badala ya 1:20.
Aidha, Mchengerwa amesema mkakati wa Serikali ni kufanya
tathmini ya ubora wa ujenzi wa matundu ya vyoo na kuendelea kutenga fedha kila
mwaka kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo kwa shule za msingi na sekondari
na kuhakikisha kuwa kwa sasa kila darasa linalojengwa kunakuwa na ujenzi wa
angalau matundu mawili ya vyoo.
“Katika mwaka 2025/26, Serikali imepanga kujenga matundu
28,580 ya vyoo yatakayogharimu shilingi bilioni 66.57 katika shule za msingi na
sekondari.”
Mchengerwa ameongeza kuwa: choo cha staha ni haki ya
mwanafunzi; ni chozi lisiloonekana, lakini lenye kuumiza.”
“Tuwashe mwenge wa
heshima shuleni-tuzime giza la aibu ya vyoo visivyofaa...Serikali haijalala
katika hili, lengo ni kuhakikisha shule zetu zinakuwa mahali salama pa
fundishia na kujifunzia," amesema.
0 Maoni