Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba barabara ambazo zipo
katika kila halmashauri ya wilaya zinafunguliwa ili kurahisisha usafiri na
usafirishaji katika maeneo ya wananchi.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi
Ibrahimu Kibassa kwenye Maonesho ya
Usalama na Afya Mahali Pa Kazi katika viwanja vya Mandewa Mkoani Singida.
Mhandisi Kibassa alisema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025
TARURA ilipangiwa kutumia Sh.bilioni 886.3 ambazo zimefanikiwa kujenga barabara
za kilometa 278.32 za kiwango cha lami na kilometa 9334 za kiwango cha
changarawe.
Aliongeza kuwa TARURA imekuwa ikitumia teknolojia ya ujenzi
wa madaraja kwa kutumia mawe ambapo yapo madaraja 401 nchini na kwa Mkoa wa
Singida yapo madaraja 34 yaliyojengwa kwa mawe na mkoa wa Kigoma unashika
nafasi ya kwanza kwa kujenga madaraja mengi ya mawe ikifuatiwa na Arusha.
"Ujenzi wa madaraja kwa teknolojia ya mawe tunatumia
sana kwasababu gharama zinapungua kwa asilimia 60 ukilinganisha na teknolojia
nyingine za kutumia kokoto kama ilivyo kawaida," alisema.
Alisema kushuka kwa gharama za ujenzi wa madaraja kwa
kutumia mawe kunatokana na kwamba mawe hayo yanapatikana kwenye mazingira ya
wananchi ambapo nao wananufaika kwa kipato na hivyo kuinua uchumi wao.
0 Maoni