Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko,
amesema dhamira ya Serikali ni kutekeleza mradi mkubwa wa Kuchakata na
Kusindika Gesi Asilia (LNG) kutokana na faida zake kiuchumi ila kwa sasa kuna
maeneo ambayo Serikali inayafanyia kazi kwa kina kupitia majadiliano na
Wawekezaji ili mradi husika uwe na tija kwa nchi na wananchi.
Dkt. Biteko ameyasema hayo jana tarehe 29 Aprili 2025
bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge
kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya
Nishati ya shilingi trilioni 2.2 kwa mwaka 2025/2026 kabla ya kupitishwa kwa
kishindo na Bunge hilo kwa asilimia 100.
“Mradi wa LNG umeanza kusemwa kwa muda mrefu na kila mmoja
angetamani mradi huu ukamilike jana lakini lazima tukubaliane kuwa lazima
tujadiliane kwa kina na wawekezaji ili kupata kilicho bora na kuleta tija,
ninachotaka kuwahakikishia ni kuwa timu ya majadiliano ya Serikali na
Wawekezaji wanaendelea na majadiliano na tunatarajia kuwa ndani ya mwaka huu
2025 kama tutakuwa tumemaliza masuala matatu yaliyosalia kujadiliwa, mkataba
huo utasainiwa ili mradi uanze mara moja,” amesema Dkt.Biteko.
Ameongeza kuwa, Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ana kiu ya
kuona mradi huo unaanza na alishatoa
maagizo kwa Wizara ya kuhakikisha kuwa mradi unaanza kutekelezwa.
Akijibu hoja kuhusu vituo vya mafuta vinavyoongezeka na
kujengwa kwa kukaribiana, Dkt.Biteko amesema kuwa Wizara ya Nishati imeanza
mazungumzo na Wizara ya Ardhi ili kuongeza umbali kati ya kituo kimoja na
kingine kutoka mita 200 za sasa kwa lengo la kuleta usalama wa watu, mazingira
na shughuli za kijamii.
Kuhusu msamaha wa kodi mbalimbali katika mnyororo wa thamani
wa gesi inayotumika kwenye vyombo vya moto kama vile magari (CNG), Dkt. Biteko
amesema kuwa Serikali ilishatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT)
kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazotumika katika mnyororo wa thamani kwa
miradi ya CNG kama vile mitungi ya CNG pamoja na vifaa vya kuwezesha kufunga
mfumo kuwezesha magari kutumia gesi hiyo.
Ameongeza kuwa, katika mwaka 2024/2025 Wizara ya Nishati
imewasilisha Wizara ya Fedha mapendekezo ya maboresho ya kodi katika gesi
asilia inayotumika kwenye magari ili kuzidi kuhamasisha matumizi ya CNG na
wawekezaji wanaowekeza kwenye miradi hiyo wapate faida na kurudisha gharama
wanazowekeza kwa haraka.
Akijibu hoja za Wabunge kuhusu gharama za kuunganisha umeme
vijijini na mijini, Dkt. Biteko amesema kuwa imeundwa timu kwa ajili ya
kuangalia namna gani gharama hizo zitapunguzwa lengo likiwa ni kuleta unafuu
kwa wananchi.
Kuhusu usambazaji wa umeme Vijijini, Dkt.Biteko amesema
kuwa, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa kwa kufikisha umeme
katika Vijiji vyote 12,318 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha
Mapinduzi ya mwaka 2020 huku kazi ya kupeleka umeme vitongojini ikiendelea kwa
kasi.
Akizungumzia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika wilaya
zote nchini kupitia mradi wa gridi imara, Dkt. Biteko amesema kuwa tayari
Serikali imeshanunua viwanja kwa ajili kujenga vituo hivyo na katika awamu ya
kwanza vitajengwa vituo 14 huku utekelezaji ukiendelea na katika laini za umeme
ambazo ni ndefu sana Serikali itaweka switching stations.
Aidha, kuhusu suala la kukatika kwa umeme nchini, Dkt.Biteko
amesema kuwa limepungua kwa asilimia 48
huku dakika za kukatika umeme zikipungua kwa asilimia 64 na kwa sasa umeme
ukikatika ni kwa sababu tu ya matengenezo ya miundombinu. Hata hivyo amesema
Serikali inaendelea kuimarisha kituo cha huduma kwa Wateja TANESCO ili taarifa ziwafikie wananchi
kwa wakati pale umeme unapokatika ikiwemo kila wilaya kuwa na kundi sogozi.
Awali, wakati wa kuhitimisha Hotuba hiyo ya Wizara ya
Nishati, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimpongeza Rais,
Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika Taifa hususan kwenye
Sekta ya Nishati akieleza kuwa moja ya misingi ya ukuaji wa kiuchumi na
maendeleo katika Taifa lolote ni uwekezaji katika Sekta ya Nishati.
Akizungumzia mikoa ambayo bado haijaunganishwa katika gridi
ya Taifa ya umeme, Kapinga alisema kuwa kuna miradi mbalimbali inayoendelea
ambapo katika Mkoa wa Rukwa kuna mradi mkubwa wa kusafirisha umeme unaoendelea
wa kutoka Iringa-Tunduma hadi Rukwa na kipande kingine cha mradi
kitakachounganisha gridi ya Tanzania na Zambia.
“Mhe.Spika katika
Mkoa wa Mtwara na Lindi tayari mkandarasi yupo eneo la kazi, mradi umeanza kwa
kujenga njia ya umeme kutokea Songea-Tunduru-Masasi hadi Mahumbika na
tumeshaanza kulipa fidia katika eneo la Tunduru hadi Masasi takriban shilingi
bilioni 4.6 na eneo lililobakia la Songea kuelekea Namtumbo na Tunduru
tutaendelea kulipa fidia ya takriban shilingi bilioni 2.7,” alisema Kapinga.
Kuhusu kupeleka gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kagera alisema
kuwa kazi inaendelea kupitia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya
Benaco-Kyaka na katika Mkoa wa Katavi mradi wa kupeleka umeme wa gridi mkoani
humo uko katika hatua za mwisho.
Akizungumzia kazi ya kupeleka umeme kwenye visiwa mbalimbali
nchini, Kapinga alisema kuwa, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 9.89
ili kupeleka mifumo ya umeme jua katika visiwa 118 ambavyo vipo katika mikoa
zaidi ya mitano hususan Wilaya ya Ukerewe.
Kuhusu maboresho miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Dar es
Salaam, Mhe. Kapinga alieleza kuwa kuna kazi zinaendelea kwa lengo la
kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika ikiwemo uboreshaji wa kituo cha
Mbagala ambacho kilikuwa na transfoma yenye uwezo wa MVA 50 lakini sasa
inawekwa transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 120 ili kukiongezea uwezo kituo
hicho ili wananchi wa Mbagala, Temeke, Yombo, Mkuranga na baadhi ya maeneo ya
Kigamboni waendelee kupata umeme wa uhakika.
Alieleza kuwa kazi hiyo imefikia mwishoni na muda wowote transfoma hiyo itaanza kufanya kazi. Kwa eneo la Kigamboni amesema maboresho pia yanaendelea kufanyika na kwamba wananchi tayari wameshaanza kuona mabadiliko ya upatikanaji umeme kupitia maboresho hayo.
0 Maoni