RC CHONGOLO: Mmefuta hasira zangu, ujenzi wa bwalo la chakula

 

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe.Daniel Chongolo, ameshindwa kuzuia hisia zake na kutamka kwa msisitizo kuwa  “ mmefuta hasira zangu” baada ya kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dkt. Samia SH iliyopo Kata  ya Namole, Halmashauri ya Mji Tunduma, Wilayani Momba.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo uliokuwa na changamoto za utekelezaji katika hatua za awali, Chongolo amesema sasa ameridhika na kazi nzuri ya usimamizi na utekelezaji unaoendelea.

"Nikupongeze sana Mkuu wa Wilaya na uongozi wa Halmashauri,  leo mmefuta hasira zangu zote kwani  nimeona na kufurahishwa na kazi nzuri ya usimamizi mliyoifanya katika mradi huu".

"Mara ya mwisho nilipokuja hapa nilikataa hata kusaini kitabu cha wageni, lakini sasa lazima mmefuta hasira zangu” alisema Chongolo.

Bwalo hilo la chakula,ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu takribani shilingi milioni 800, awali utekelezaji wake ulianza kwa kusuasua, jambo lililomkera kiongozi huyo wa mkoa.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa ameutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha ifikapo Aprili 25, bwalo hilo linaanza kutumika rasmi, huku akiahidi kushiriki chakula cha pamoja na wanafunzi kama ishara ya mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tunduma, Mariamu Chaurembo, amesema tayari Halmashauri imefanya mabadiliko ya bajeti na kutenga shilingi milioni 350 kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki.

Amesema bwalo hilo linatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi milioni 800 hadi kukamilika kwake, na kuahidi kuwa mradi huo utakamilishwa kwa viwango na muda uliopangwa.

Mhe. Chongolo amefanya ziara ya siku moja ya kutembelea Halmashauri hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Halmashauri za mkoa kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo.



Chapisha Maoni

0 Maoni