Bunge laelezwa ujenzi mradi wa EACOP wafikia asilimia 55

 

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeelezwa kwamba Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania (EACOP) unaoendelea kutekelezwa ujenzi wake umefikia asilimia 55.

Hayo yameelezwa Bungeni leo Aprili 28, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwasilisha Hotuba ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa mwaka 2025/2026.

Dkt. Biteko amezitaja kazi zilizotekelezwa kuwa ni pamoja na kukamilika na kuanza kazi kwa karakana ya kuweka mfumo wa joto kwenye mabomba (Thermal Insulation System (TIS) Plant) pamoja na kuwasili nchini kwa mabomba yenye uwezo wa kujenga kilomita 900.

Kazi nyingine ni kuwekwa mfumo wa kuhifadhi joto katika mabomba yenye urefu wa kilomita 443.66; kupelekwa kwenye maeneo ya mradi kwa mabomba yenye mfumo wa kuhifadhi joto yenye uwezo wa kujenga kilomita 364.3.

Pia, Mhe. Dkt. Biteko ameeleza kwamba kazi ya kuendelea kwa ujenzi wa matenki manne (4) katika eneo la Chongoleani imefikia asilimia 74.2; na ujenzi wa jeti ya kupakilia mafuta ambao umefikia asilimia 69.1.

Chapisha Maoni

0 Maoni