ZAIDI ya leseni 4,000 za uchimbaji madini zipo katika
utaratibu wa kutolewa katika maeneo manne ya Mkoa wa Kimadini Mbogwe mkoani
Geita, huku wazawa na wawekezaji kutoka nje wakitakiwa kuchangamkia fursa
zilizopo mkoani humo.
Akizungumza katika mahojiano, Afisa Madini Mkazi wa Mbogwe,
Mhandisi Jeremiah Hango amesema maeneo yaliyotengwa ni Nyamikonze ambapo leseni
81 ziliweza kugawiwa kwa wachimbaji madini wadogo, huku eneo la Mwamakiliga zikitegwa
leseni 27.
“Maeneo mengine ni Bukombe kijijini leseni 140 na sasa hivi
mchakato wa Kigosi ambapo takribani leseni 4,000 za uchimbaji madini zimeshatengwa,”amesema
Mhandisi Hango.
Amesema, zoezi la ugawaji bado linaendelea na kwamba fursa
zilizopo zikitumiwa vizuri serikali itaweza kukusanya kiasi kikubwa cha
maduhuli.
“Nawakumbusha wamiliki wa leseni ambao wameshikilia leseni
katika mkoa wetu wa kimadini Mbogwe wazifanyie kazi leseni hizo, nyingi
hawazifanyii kazi, kuna leseni za utafiti ambapo ukienda saiti watu wanaofanya
utafiti ni wachache sana, amesema Mhandisi Hango na kuongeza,
“Vile vile niwakumbushe kama leseni hizo hawatazifanyia kazi
tutazifuta na kuwapa watu wengine wenye nia ya kufanyia kazi leseni na sio
kuzishikilia.”
Aidha, amesema, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia
sekta ya madini katika Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali
yamekuwa yakiongezeka kila mwaka tangu mkoa huo wa kimadini ulipoanzishwa mwaka
2021.
“Mwaka 2021/2022 tuliweza kukusanya Shilingi Bilioni 21, mwaka
2022/2023 tulikusanya Shilingi Bilioni 22, mwaka wa fedha uliopita 2023/2024 tumekusanya
Shilingi Bilioni 27 mwaka huu wa fedha
mpaka sasa hivi tumeweza kukusanya Shilingi Bilioni 22,”amesema Mhandisi Hango
na kuongeza.
“Tunaamini kwa mwelekeo huu tunaoenda nao mpaka kufikia
mwishoni mwa mwaka tutaweza kuzidi lengo tulilokusanya katika mwaka wa fedha
uliopita,” amesema.
Ameendelea kusema kuwa asilimia 90 ya
madini yanayochimbwa Mbogwe ni dhahabu, yapo pia madini ujenzi.
“Mapato ya Mbogwe asilimia 60 tunayapata katika wilaya ya
Nyang’wale ndiko uchimbaji wa madini kwa kiasi kikubwa unafanyika, lakini kuna
juhudi ambazo zinafanyika kwa upande wa Serikali kuhakikisha uwezeshwaji wa
wachimbaji kuzitumia fursa zilizopo.
“Tuna fursa nyingi katika mkoa wetu wa kimadini Mbogwe, kuna fursa ya biashara ya madini, tuna masoko mawili ya Nyang’wale na Masumbwe, wafanyabiashara wakubwa wa madini ‘dealers’ wenye uwezo wa kununua hii dhahabu waje waombe leseni.
Pia, amesema kuna fursa ya ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji wa madini ambapo kwa sasa ni michache kwa maana wachimbaji wamehamasika kuachana na matumizi ya zebaki kwenda kwenye matumizi ya mitambo ya kuchenjulia ya CIP.



0 Maoni