Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Barbados, Mhe. Mia
Mottley ambapo wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi
hizo mbili.
Mazungumzo hayo yamefanyika
katika makazi rasmi ya Waziri Mkuu, Mhe. Mia Mottley, Jijini
Bridgestone, nchini Barbados.
Waziri Mkuu Mia amesema, kuna umuhimu wa kuwa na mkakati wa
pamoja na kushirikiana kwa lengo la kukuza utalii kati ya Barbados na Tanzania
na nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla. Amesema kuna maeneo mengi ya vivutio
vya utalii ambavyo vinaweza kuzinufaisha pande hizo mbili yakiwemo masuala ya
ukarimu.
Maeneo mengine ya ushirikiano ni katika utoaji wa mafunzo
maeneo ya ufundi kati ya nchi za Carib (Caribbean) na nchi mbalimbali za
kiafrika huku akisisitiza kuwa umuhimu wa uboreshaji wa masoko na kubadilishana
wataalam katika sekta mbalimbali kwa makubaliano maalum.
Aidha, amesema upo uhitaji wa wataalam katika sekta ya maji
na miundombinu na hivyo kuna uwezekano wa kubadilishana wataalam ili kujengeana
uzoefu katika sekta mbalimbali kulingana na makubaliano yatakayofikiwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,
Mhe. Dkt. Biteko amesema mapendekezo hayo ni mazuri na yanaweza kuwa matokeo
chanya baada ya kuchambuliwa na watalaam katika sekta husika kupitia Wizara
zinazohusika na masuala ya kidiplomasia.
Dkt. Biteko amesema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa
Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza kampeni ya Nishati Safi
ya Kupikia ambayo inalenga kuwawezesha asilimia 80 ya watumiaji wa nishati
kuondokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi ifikapo mwaka 2034.
Katika utekelezaji wa mpango huo, amesema Tanzania inatembea
kifua mbele kunadi mkakati huo wa miaka 10 ambao pamoja na mambo mengine
unakusudia kupunguza madhara kwa watumiaji wa nishati isiyokuwa safi
inayopelekea uchafuzi wa mazingira, magonjwa ya kupumua pamoja na vifo.
“Januari mwaka huu tumekuwa na mkutano wa Wakuu wa nchi za
Afrika (M300) uliofanyika jijini Dar es Salaam ukilenga kuwa wezesha watu
milioni 300 barani Afrika ambao hawajaona umeme kuweza kupata haki hiyo ikiwa ni
miaka mitano kuanzia sasa na baada ya hapo itaweka namna tunavyoweza kusonga
mbele kulingana na matokeo yanayofikiwa,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amefafanua kuwa, hatua ya Tanzania kushiriki
katika mkutano wa nishati endelevu kwa wote (SEforALL) uliofanyika nchini
Barbados, ni kuthibitisha nia yake thabiti inayolenga matokeo chanya. Hivyo,
amesema yapo maeneo mengi ya kushirikiana na kuwezesha wananchi wa pande zote
mbili kupata maendeleo na ustawi wa pamoja.
Mkutano wa Dkt. Biteko Waziri Mkuu wa Barbados, umehitimisha
ziara ya kikazi nchini humo ambako alishiriki katika Kongamano la kimataifa la
nishati endelevu kwa wote pamoja na mikutano ya wadau mbalimbali iliyojikita
katika uboreshaji wa sekta ya nishati kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,
alifuatana na Waziri wa Maji, Nishati na Mhe. Shaib Kaduara, Balozi wa Tanzania
nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha.
Felichesmi Mramba na Mshauri wa Rais katika masuala ya Nishati na Maendeleo ya
Jamii, Mhe. Angellah Kairuki.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




0 Maoni