Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake
Duniani, wanawake zaidi ya 400 kutoka taasisi za serikali na sekta binafsi wemetembelea
hifadhi ya Ngorongoro na kushuhudia vivutio mbalimbali ikiwemo wanyama wakubwa
watano maarufu kama "Big Five".
Akizungumza na wanawake hao baada ya kuwapokea jana Machi 7,
2025 Kamishina Msaidizi Mwandamizi anayesimamia idara huduma za Utalii na
Masoko, Mariam Kobelo amesema ujio wa wanawake hao utaendelea kuhamasisha
utalii wa ndani kwenye vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo.
"Tukiwa tunaelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya
siku ya wanawake Duniani, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) tunatumia
fursa hii kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya Eneo la Hifadhi, na
Leo kwa kushirikiana na Kampuni ya Utalii ya Tanzanite Cooperates tumepokea wanwake
takriban 400 waliokuja kutalii,"alisema Mariam.
Aidha, Mariam alisisitiza kuwa NCAA imejiandaa vyema
kuhakikisha kuwa ziara hiyo ya kitalii itatumika kuleta chachu kwa watanzania
wengine ikiwa ni jitihada za Kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii
vilivyopo nchini.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya kitalii ya Tanzanite
Cooperates, Bi. Elina Mwangomo alisema kwamba Kampuni yake imejikita zaidi
kwenye utalii wa ndani na imekuwa ikifanya ziara za kutembelea Hifadhi
mbalimbali nchini ambapo bonde la kreta limekuwa sehemu pekee ambapo watalii
wanaweza kujionea wanyama wengi kwa karibu zaidi ndani ya muda mfupi.
" Kreta ya Ngorongoro ni sehemu pekee ambako watalii
wetu wengi wamekuwa wakivutiwa kuja kutembelea na kwa muda sasa tumekuwa tukija na makundi mbalimbali na Leo
tuko na kundi la takriban wanawake 400
ambao tumekuja kutalii na kufurahi pamoja tukielekea kilele cha maadhimisho ya
siku ya Wanawake duniani,” alisema Elina
Kwa upande wake Bi.Gloria Mziray kutoka Mfuko wa taifa wa bima ya Afya (NHIF) Arusha
ambaye ni mmoja kati ya wanawake waliokuwa kwenye ziara hiyo alieleza kuwa
safari yao ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ya kipekee sana na
wamefurahishwa kuona wanyama mbalimbali waliopamba hifadhi hiyo wakiwa kwenye
Mazingira yao ya Asili.
Bi. Fatuma Abduli kutoka benki ya CRDB ambao wamekuwa wadau
wakubwa wa utalii nchini pamoja na kufurahishwa na upekee wa Kreta ametoa wito
kwa watanzania kujenga hulka ya kutembea vivutio mbalimbali vilivyopo ndani ya
nchi.
Wakiwa katika hifadhi hiyo wanawake hao pamoja na watalii
wengine waliotembelea maeneo ka Kreta ya Ngorongoro na tambarare za Ndutu
wameshuhudia vivutio mbalimbali ikiwemo wanyama wakubwa maarufu kama "Big
Five" ambao ni Faru, Tembo, chui, Nyati na Simba.
Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kinafanyika leo Machi 08, 2025 Mkoani Arusha ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Na. Philomena Mbirika- Ngorongoro Kreta
0 Maoni