Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.
Dkt. Hussein Mwinyi amezihamasisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na
Mifuko ya Maendeleo ya Petroli (Petroleum Fund) ambayo itasaidia katika utafiti, ubunifu, mafunzo na uendelezaji
wa Sekta ya Mafuta kwa ujumla.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 07 Machi 2025 jijini Dar
es Salaam wakati akifunga Kongamano na
Maonesho ya Petroli Afrika Mashariki (EAPCE’25) ambalo limefanyika kwa Siku
Tatu.
Ameeleza kuwa, Dira ya Afrika Mashariki ya 2050 inaelekeza
kuhusu kuanzishwa kwa Mfuko huo wa Petroli hivyo huu ni wakati muafaka wa kutekeleza suala hilo
kama lilivyoainishwa katika Ibara ya 114 ya Mkataba wa Afrika Mashariki ambayo
inaelekeza kuimarisha mashirikiano katika kusimamia rasilimali kwa faida ya
wote.
“Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimejifunza
kutoka Umoja wa Wazalishaji wa Mafuta
Afrika (APPO) kwa kushirikiana na Benki ya Afrexim ambao wamekubaliana
kuanzisha Benki ya Nishati ya Afrika (AEB) ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ufadhili ya miradi ya
mafuta na gesi kwa kigezo cha kuchangia katika mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Dkt.Mwinyi.
Rais Mwinyi pia ameeleza kuhusu umuhimu wa Rasimali za
Mafuta na Gesi Asilia kuwa na mchango katika ukuaji wa Sekta nyinginezo
akitolea mfano jinsi Sekta ya Mafuta nchini ilivyosaidia miradi ya umeme hasa
usambazaji wa umeme vijijini.
Aidha, amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa
kujitolea kwake bila kuchoka katika maendeleo ya sekta zote ikiwemo mafuta na
gesi ambapo chini ya uongozi wake miradi ya kimkakati katika Sekta hiyo
imeendelea kutekelezwa.
Pia, amezipongeza
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanya mkutano
huo kwa mafanikio ikiwemo
Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamati ya kitaifa ya EAPCE
2025, Timu ya Kitaifa ya Uratibu na kamati zake ndogo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,
Mhe.Dkt. Doto Biteko amesema Mkutano huo
umehusisha majadiliano, kubadilishana mawazo, kuwasilisha mawasilisho kutoka
kwa Wataalam wa Sekta ya Mafuta na Gesi na kuangazia namna bora kutumia
rasilimali za mafuta kuhakikisha
kunakuwa na upatikanaji wa uhakika, nafuu na usalama wa nishati.
Amesema Kongamano la EAPCE’25 limehudhuriwa na washriki zaidi ya 1400 kutoka nchi 25 na huo ni ushuhuda wa dhamira ya dhati ya nchi wanachama wa EAC kukuza ajenda ya nishati ya uhakika kwa maendeleo endelevu ya watu.
0 Maoni