Wafanyakazi wa Shamba la Miti Meru-Usa, wakiongozwa na
Mhifadhi Mkuu PCO Ali D. Maggid, wameadhimisha Siku ya Misitu Duniani na
Upandaji Miti Kitaifa kwa kupanda miti katika eneo la Safu ya Themi ndani ya
shamba hilo.
Katika zoezi hilo lililofanyika jana, jumla ya hekta 38.3 za
ardhi zimepandwa miti, huku miche 42,551.3 ikipandwa katika juhudi za kuhifadhi
mazingira na kulinda vyanzo vya maji.
Katika kampeni hiyo, PCO Maggid alishirikiana na wananchi wa
vijiji vya Bangata, Midawe, na Ng’resi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa
kuhamasisha ushirikiano wa jamii katika utunzaji wa mazingira.
Hifadhi ya Shamba la Miti Meru-Usa ni chanzo kikuu cha maji
kwa wakazi wa Arusha, na hivyo upandaji miti umeelezwa kuwa ni hatua muhimu
katika kuhakikisha upatikanaji wa maji na kupambana na athari za mabadiliko ya
tabianchi.
Wananchi walioshiriki zoezi hilo walieleza umuhimu wa
kuhifadhi misitu kwa maisha yao ya kila siku.
“Misitu ndiyo inatusaidia kupata mvua na maji kwa ajili ya
kilimo na matumizi ya nyumbani. Kupanda miti leo ni jambo kubwa kwetu, na
tunajivunia kushiriki,” alisema Julius Laizer, mkazi wa Kijiji cha Bangata.
Naye Mama Amina John, mkulima kutoka Kijiji cha Midawe,
alisisitiza kuwa jamii inapaswa kuchukua hatua za haraka kuzuia ukataji miti
holela.
"Tunahitaji zaidi elimu kuhusu uhifadhi wa misitu,
lakini pia mbegu za miti zinazofaa kwa maeneo yetu,” alisema.
Kwa upande wake, PCO Maggid alieleza kuwa moja ya faida kubwa za uhifadhi wa misitu ni kuchochea upatikanaji wa mvua, jambo linalosaidia uzalishaji wa chakula duniani. Aliwataka wananchi kuendelea kushiriki katika juhudi za upandaji miti ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.
0 Maoni