Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wanafunzi wa
shule zote nchini kuwatunza, kuwapenda na kuwajali wanafunzi wenzao wenye
mahitaji maalum ili nao waweze kutimiza ndoto zao.
Amesema Serikali imejenga miundombinu bora ambayo sasa
inawawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kusoma na kufaulu na kupata nafasi
katika shule mchanganyiko na hivyo ni wajibu wa wanafunzi wengine kuwapenda na
kuwasaidia.
"Nimevutiwa namna mnavyowajali na kuwapenda wanafunzi
wenzenu wenye mahitaji maalum, ninaomba muendelee na upendo huo muwathamini na
kuwapenda ili nao watimize ndoto zao."
Ameyasema hayo leo, (Jumamosi Machi 22, 2025) alipotembelea
Shule ya Sekondari ya Mkoa ya Wasichana ya Njombe iliyoko Wilaya ya
Wanging'ombe Mkoani Njombe.
Mheshimiwa Majaliwa amesema pamoja na mambo mengine
ameridhishwa na ujenzi na mandhari ya shule hiyo na zaidi amevutiwa na mifumo
ya TEHAMA iliyoko katika shule hiyo.
"Nimevutiwa na mindombinu ya TEHAMA iliyopo katika
shule hii, wanafunzi mhakikishe mnaitunza
ili iwe na tija na kutimiza malengo yenu ya kujisomea."
Amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa
katika shule za wasichana kwa kujenga shule kubwa zenye viwango mikoa yote
nchini ikiwa ni maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya
uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya elimu na hakika sasa tunaona matunda ya
uwekezaji huo."
Naye, Naibu Waziri OR-TAMISEMI, na Mbunge wa Jimbo la
Wanging'ombe Festo Dugange, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa shule hiyo
sambamba na miradi mingine mingi ya maendeleo ikiwemo vituo vya afya, huduma za
maji na miundombinu ya barabara.
Shule hiyo imegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 4 ina vyumba vya madarasa 22, mabweni 9, bwalo na jiko pamoja na miundombinu mingineyo tayari imedahili wanafunzi 460 wa michepuo mbalimbali ya masomo.
0 Maoni