Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
amesema wakazi wa Wilaya ya Ruangwa hawana deni na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa
aliyoifanya wilayani humo.
Amesema Rais Dkt. Samia ametoa fedha nyingi za kutekeleza
miradi ya maendeleo kwenye sekta za kilimo, afya, elimu, miundombinu na
nyinginezo.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, 15 Machi 2025) wakati
akizungumza katika mkutano wa hadhara na wanakijiji wa kijiji cha Narungombe, Wilayani
Ruangwa.
"Rais Dkt. Samia amewezesha kupatikana kwa fedha za
kutekeleza miradi ya maendeleo nchini ikiwemo kwenye wilaya yetu ya Ruangwa,
Tunaachaje kumuunga mkono kwa kazi kubwa aliyoifanya."
Amesema Wana-Ruangwa wanatoa shukrani za dhati kwa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyotoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali
ya maendeleo wilayani humo.
"Wilaya yetu ilikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji
wa maji kutokana na kuwa na chumvi nyingi chini inayotokana na sababu za
kijiografia lakini Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha maji safi na
salama yanapatikana."
Amesema Serikali iko katika hatua za utekelezaji za mradi
mkubwa wa maji wa shilingi bilioni 119 kutoka mto Nyangao, kuja vijiji 34
vya Ruangwa ambao utahakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika wilayani humo.
"Nitaendelea kufanya kazi na nyie usiku na mchana, jua
kwa mvua hadi kuhakikisha Ruangwa inafanikiwa zaidi,”
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameshuhudia
wanachama 24 wa Chama cha ACT Wazalendo wakijiunga na Chama cha Mapinduzi
(CCM).
Miongoni mwa wanachama hao ni pamoja na Aliyekuwa Katibu
Mwenezi wa ACT Wazalendo Wilaya ya Ruangwa, Hammis Selemani Chikanga, Diwani wa
Kata ya Mbwemkuru Ismail Ali Mbwerei, Katibu wa Vijana Omary Kitunguu, pamoja
na wanachama wengine.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake Aliyekuwa Katibu
Mwenezi wa ACT Wazalendo Wilaya ya Ruangwa Hammis Chikanga, Amesema sababu za
wao kujiunga na CCM ni kuunga mkono jitihada na kazi kubwa inayofanywa na Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia inafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi na inaleta miradi na mambo mengi kwa wananchi hivyo tukiendelea kuwapinga na kuwakosoa tutakuwa hatuwatendei haki."



0 Maoni