Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Musa Kuji amewataka Maafisa na
Askari wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo kufanya kazi kwa
uadilifu, weledi, bidii, nidhamu pamoja na ushirikiano ili kutimiza adhima na
malengo ya kuimarisha shughuli za uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha
Rubondo.
Kamishna Kuji aliyasema hayo jana Machi 15, 2025 alipofanya
ziara ya kikazi ya kukagua shughuli mbalimba na kufanya kikao na Maafisa na
Askari hao katika ofisi za Makao Makuu ya hifadhi hiyo yaliyopo eneo la Kageye
ndani ya Hifadhi hiyo iliyopo katika Mkoa wa Geita.
“Ninawapongeza sana Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa
Kisiwa cha Rubondo kwa kuchapa kazi na niendelee kuwasisitiza tuongeze bidii
katika utendaji wa kazi na pia tuendelee kufanya kazi kwa nidhamu, uadilifu na
ushirikiano ili kuimarisha ulinzi wa maliasili za Taifa” alisema Kamishna Kuji
Akizungumza katika kikao hicho Kamishna Kuji alieleza
dhamira ya Shirika ni kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi.
“Shirika letu litahakikisha linaendelea kuimarisha maslahi
ya watumishi ikiwemo kuzingatia haki ya kujiendeleza kielimu, kutoa matibabu
stahiki kwa mtumishi na wategemezi wake, haki ya watumishi kupandishwa vyeo
pale vigezo vyote vinapokuwa vimezingatiwa na haki ya mtumishi kusikilizwa na
kuthaminiwa,” aliongeza Kamishna kuji.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Iman Kikoti, ambaye
ndiye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo alimshukuru Kamishna Kuji kwa
kutenga muda wake na kufanya ziara katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo
ili kujionea shughuli zinazotekelezwa na hifadhi pamoja na kupokea changamoto
za watumishi pamoja na kupata taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa majukumu
ya kulinda, kusimamia na kuhifadhi maliasili zilizopo katika Hifadhi.
“Hali ya uhifadhi inaendelea vizuri ambapo doria zinafanyika
vizuri na idadi ya watalii imeongezeka ambapo hadi sasa tumepokea zaidi ya
watalii 2,076 kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025. Tutaendelea kufanya kazi kwa
bidii na nidhamu ili kufikia lengo la kuongeza idadi ya watalii na mapato,”
alieleza Kamishna Dkt. Kikoti.
Naye, Askari Uhifadhi Daraja la Kwanza Hiza Joseph Mahanyu
alibainisha furaha yake kwa Kamishna Kuji kutembelea Hifadhi ya Taifa Kisiwa
cha Rubondo.
“Afande tunakushukuru sana kwa kuja kututembelea na
tumefurahi sana kwani ujio wako ni alama dhahiri kuwa unajali na kuthamini
mchango wa mtumishi mmoja mmoja katika kutekeleza majukumu ya kulinda maliasili
za Taifa hususan ni watumishi tuliopo katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha
Rubondo,” alieleza Mahanyu.
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo ni moja kati ya Hifadhi
za Taifa zilizopo katika Kanda ya Magharibi yenye sifa ya kuwa na wanyama adimu
kama Sokwe, shughuli mbalimbali za utalii ikiwemo utalii wa matembezi ya miguu,
matembezi ya kutumia boti, mchezo wa kuvua na kuachia Samaki (Sport Fishing),
utalii wa kutembea kwa gari na utalii wa kushiriki zoezi la kuzoesha sokwe
(Chimpanzee Habituation Experience).
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo ni miongoni mwa kivutio kikubwa cha Utalii katika ukanda wa Ziwa Viktoria ambayo inasifika kwa kuwa na wanyama adimu aina ya sokwe mtu pamoja na kuhifadhi msitu mkubwa wa asili ya Congo (Low Congolese Forest).



0 Maoni