Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri
Serikali kutafuta fedha za kuwalipa fidia wananchi waliopitiwa na Miradi ya
kufua Umeme ya Ruhudji na Rumakali, ili wananchi hao wapishe maeneo hayo na
waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku wakati miradi hiyo ikisubiri
kutekelezwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni
Mbunge wa Same Magharib Mhe. David Mathayo baada ya kupokea taarifa ya
utekelezaji wa miradi ya umeme katika Mkoa wa Njombe, tarehe 16 Machi 2025.
Mhe. Mathayo amesema, Serikali itafute fedha za kuwalipa
fidia wananchi walioathiriwa na miradi hiyo ili wananchi hao wapishe na meneo
hayo na waendelee na shughuli zao zingine wakati serikali ikiendelea kutafuta
fedha za kutekeleza miradi hiyo.
“ Tayari tathmini imeshafanyika kwa wananchi watakaopitiwa
na mradi huo na gharama za kuwalipa zimefahamika,na wananchi wanayo hiyo
taarifa, ni vyema sasa serikali ikatafuta fedha za kuwalipa fidia wananchi hao
ili wakaendelee na Maisha yao mengine wakati juhudi za kutekeleza mradi hiyo
zikiendelea kufanyika,” alisisitiza Mhe. Mathayo.
Utekelezaji wa Miradi ya Ruhudji na Rumakali utaiwezesha
nchi kupata zaid ya megawati 500 za umeme ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya
Taifa na kuimarisha hali ya upatikanai wa umeme nchini.
Kamati hiyo imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupelekea umeme kwa
wananchi wake kama alivyoahidi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kusema
kuwa ni jambo la msingi sana kwa kuwa wananchi wamekuwa wakisubiri umeme huo
kwa muda mrefu na kwa miaka mingi.
Alifafanua kuwa kuna maeneo mengine ni magumu kufikika kwa
kuwa hakuna miundombinu ya Barabara na ambayo wananchi wake walikuwa hawajawahi
kupata huduma ya umeme tangu enzi za uhuru, lakini kwa sasa wamepata umeme
kutokana na umakini wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwajali wananchi wake.
Pamoja na mambo mengine amewapongeza Wakala wa Nishati
Vjijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kupelekea umeme katika
Vijiji na Vitongoji vya Mkoa huo ambapo katika maeneo mengine umeme huo
umefikishwa kwa asilimia mia moja licha ya kuwa na miundombinu hafifu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith
Kapinga, akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.
Dkt. Doto Biteko, amesema Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zilizo chini yake
wamepokea maelekezo ya kamati hiyo pamoja na shukrani kwa niaba ya serikali,
katika kutekeleza miradi ya umeme.
Ameweka wazi kuwa shukrani hizo zinakwenda moja kwa moja kwa
Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,kwa kuwa ndiye amekuwa kinara katika
kuhakikisha kuwa miradi ya Umeme inatekelezwa na inafahamika duniani kote kwa
namna ambavyo anasimamia Nishati kwa kadri ya uwezo wake ili wananchi wengi
wafikiwe na umeme.
Kuhusu suala la fidia amesema kuwa Serikali imekuwa ikilipa
fidia kwa wananchi wote wanaopisha miradi mbalimbali inayoanzishwa nchini,
ikiwemo hiyo ya Ruhudji na Rumakali yenye thamani ya shilingi Bilioni 63.
Akitolea mfano baadhi ya miradi ambayo wananchi wake
wamelipwa fidia ni pamoja na ule ya Tanzania - Zambia (TAZA), na mradi wa
kupelekea umeme wa Gridi mkoani Katavi.
Serikali ya imepanga kuhakikisha wananchi wake wanaendelea
kupata umeme wa uhakika na katika Mkoa wa Njombe zaidi ya asilimia 98 ya vijiji
vyote vina umeme ambapo vimebaki Vijiji tisa tu ambavyo changamoto zake
zinatatuliwa ili navyo vipate umeme na kuongeza kuwa Pia wataendelea kusambaza
umeme katika maeneo ya pembezoni na kuimarisha nguvu ya umeme ili wananchi
wapate umeme mwingi wa kutosha kukidhi mahitaji yao.
Azma ya serikali ni kuhakikisha kuwa ikifikapo 2030 asilimia
75 ya wananchi wote nchini wawe wamepata umeme na waweze kutumia nishati safi
ya kupikia.
“Kwa sasa Serikali iko hatua za mwisho katika kukamilisha
mradi wa Julius Nyerere utakaozalisha Megawati 2,115, hivyo hivi karibuni it’s
za kutekeleza miradi ya Ruhuji na Rumkali, azma ya serikali ni kuhakikisha
inaongeza vyanzo vya uzalishaji wa umeme hivyo serikali inatafuta fedha ili
kuanza utekelezaji wa miradi hiyo,” alisema Kapinga.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati
Vijijini REA, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwa mwambao wa Ziwa Nyasa una
maeneo korofi ambayo hayafikiki kirahisi katika utekelezaji wa mradi wa
usambazaji umeme vijijini kwa kuwa hakuna miundombinu ya Barabara na kuahidi
kutafuta utaratibu maalum wa kumpata mkandarasi mahsusi wa kutekeleza kazi hiyo
ambapo sasa kazi kufanya upembuzi yakinifu inaendelea.
Amesema baada kukamilika kazi ya kusambaza umeme katika
maeneo hayo, itaanza na itakamilika kabla ya kufika mwezi wa Sita mwaka huu
2025 ambapo vijiji hivyo vyote vitakuwa vimewashwa Umeme.
Kwa upade Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme
Nchini (TANESCO) Renata Ndege amesema, miradi hiyo ya Ruhuji na Rumakali
itagharimu zaidi ya shilingi trilioni 4 kutekeleza miradi hiyo.
Miradi hiyo ikitekelezwa itaongeza upatikanaji wa umeme nchini pia itaboresha maendeleo ya uchumi, Ajira kwa wananchi,miundombinu ya barabara, pamoja na huduma za kijamii.



0 Maoni