WACHIMBAJI wadogo wa madini wilayani Nyang’wale wameishukuru
Serikali kwa kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji ambao wanatoa msaada
wa kiufundi ambapo elimu ya uchimbaji na vifaa vimetolewa kwa wachimbaji hao.
Lengo ni kuwatoa kwenye uchimbaji mdogo na kuwa uchimbaji wa kati na baadaye
mkubwa.
Akizungumza katika mahojiano, mmoja wa Wakurugenzi wa Mgodi
wa Dhahabu wa Igalula, Jumanne Misungwi amesema
mgodi huo ulipewa leseni mwaka 2019 lakini kulikuwa na changamoto za
uzalishaji kutokana na kutokuwa na vifaa vya kisasa.
“Hatukuwa na teknolojia ya uzalishaji mwaka jana mwishoni
tukaingia makubaliano na mwekezaji Zhong Tan Kun kwa utaratibu wa ‘Technical
Support’, mfumo uliowekwa na Rais Dk.
Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya
kutusaidia wachimbaji wadogo, kwa sababu wao wana vifaa vingi, mkataba ni wa miaka
mitatu,” amesema Misungwi.
Amesema tangu wawekezaji hao waanze kazi imetimia miezi
saba, lakini miezi ya uzalishaji ni miwili mpaka sasa na kuongeza kuwa tayari
wamezalisha zaidi ya kilo 15 za dhahabu.
“Tunajivunia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wetu
Anthony Mavunde, sisi wachimbaji hatuoni haya kusema mitano tena,’’ amesema
Misungwi na kuongeza.
“Waziri Mavunde tunajivunia nae sana amekuwa akishirikiana
na sisi bega kwa bega kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini ya Mbogwe hakika
tunaona manufaa ya uwekezaji.’’
Aidha, amesema kupitia uwekezaji katika mgodi huo wameweza
kujenga Shule ya Sekondari inayofahamika kwa jina la Igalula Secondary-Gold
Mine, ambayo imetokana na mgodi huo wa Igalula.
“Hii shule imetokana na mgodi wetu sisi wazawa, sasa hivi tunaendelea na ujenzi
wa maabara katika shule hiyo.
"Kampuni imetoa ajira kwa wazawa, Rais Samia mitano
tena. Uzalishaji ulikuwa mdogo kwakuwa mwamba wetu ni mlaini sana hautulii,
haukuwa rafiki, wataalam kutoka Madini Mbogwe wakatushauri tuingie mkataba na
kampuni hiyo kwa ajili ya msaada wa kiufundi ‘technical support’.
Kwa upande wa mwekezaji wa mgodi wa Igalula kutoka China,
Liu Diheng amesema wameamua kuwekeza katika Sekta ya Madini Igalula kutokana na
ushirikiano mkubwa wa kimahusiano uliopo kati ya Serikali ya China na Tanzania
kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa China Xi
Jinping .
“Tumekuja kwa wingi kuwekeza Tanzania kutokana na historia
ya kimahusiano iliyopo, tunawafundisha wazawa mbinu mbalimbali za kiufundi
katika uchimbaji madini na vifaa, mwisho wa siku wananchi wa mataifa haya
mawili, Tanzania na China wote tupate chochote kitu,”amesema Liu.
Nae, Juma Mashimba, Katibu Mkuu wa Kikundi cha Utulivu
Mining Group kilichopo kijiji cha Bululu
Kata ya Nyamtukuza wilayani Nyang’wale Mbogwe mkoani Geita, amesema kikundi
hicho kinaundwa na vikundi 16 vyenye wanachama 600 na walianza uchimbaji mwaka 2019 lakini uchimbaji haukuwa
na tija kutokana na ukosefu wa vifaa, ulikuwa umedorora ambapo hadi mwaka jana
walikuwa wamezalisha kilogramu 9.7 pekee.
“Lakini mwaka 2024 mwishoni tukatafuta mwekezaji kampuni ya
Zhongtan Longten Kuangye Mining ambaye tuliingia naye ubia kupitia utaratibu wa
‘technical support’.
“Mchakato kidogo ulikuwa shida wachimbaji baadhi waligomea,
Mheshimiwa Waziri Mavunde akaingilia kati
kutatua, mgogoro ukaisha tukaanza uzalishaji, mpaka sasa tumeshazalisha
kilo 24 za dhahabu, tumelipa mrabaha wa Serikali zaidi ya milioni 280, TRA
zaidi ya milioni 90 na halmashauri zaidi ya milioni 15,” amesema Mshimba.
Amesema, wamepata mafanikio makubwa tofauti na walivyokua
wanachimba awali na kuendelea kufafanua, “Tunashukuru Serikali kutuletea wawekezaji
kama hawa angalau sasa kipato chetu kidogo kimeongezeka.”
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Kikundi cha Group 9 Mining
Company Limited, Costatine Mazinzi amesema walipewa leseni ya uchimbaji Desemba
mwaka 2019 ambapo awali walikuwa wanafanya uchimbaji mdogo wa maduara hivyo
mwaka jana wakaingia mkataba na wawekezaji 'technical support' ili kuongezea
maarifa ya uchimbaji, mkataba ni miaka mitatu ambapo mwishoni mwa mkataba
wataweza kujisimamia wenyewe.
Aidha, amesema kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya ujenzi, kufikia mwezi Mei mwaka huu, wataanza uzalishaji, ambapo matarajio yao ni kuzalisha si chini ya kilo 20 kwa mwaka.



0 Maoni