Serikali inaendelea na juhudi za kulinda rasilimali za
misitu nchini, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii
anayeshughulikia Maliasili, CP Benedict Wakulyamba, leo ametembelea Msitu wa
Hifadhi wa Bondo uliopo kati ya Wilaya ya Handeni na Kilindi.
Ziara hiyo iliyofanyika jana imelenga kutathmini utekelezaji
wa hatua za kulinda hifadhi hiyo dhidi ya uvamizi na uharibifu wa mazingira.
Katika ziara hiyo, CP Wakulyamba aliambatana na Kamishna
Msaidizi wa Kanda ya Kaskazini, SACC James Nshare, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya
Kilindi, DC Hashim Mgandilwa, wahifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS) kutoka Handeni na Kilindi, na viongozi wa usalama wa eneo hilo.
Ziara hiyo imejikita katika kukagua maeneo yaliyowahi kuwa
na makazi ya watu waliovamia hifadhi hiyo na tathmini ya utekelezaji wa zoezi
la kuwaondoa (eviction). Aidha, ameangalia mipaka ya msitu wa Bondo, uwekaji wa
mabango ya hifadhi, na mikakati ya kudhibiti uharibifu wa mazingira.
“Serikali haitarudi nyuma katika kulinda misitu yetu dhidi
ya uharibifu. Hifadhi ya Bondo ni mojawapo ya maeneo muhimu ya bioanuwai, na
tunahakikisha kuwa sheria za uhifadhi zinatekelezwa ipasavyo,” alisema CP
Wakulyamba wakati wa ukaguzi huo.
Msitu wa Bondo, ambao ni mojawapo ya vyanzo muhimu vya maji
na makazi ya viumbe hai, umeendelea kukabiliwa na changamoto za uvamizi na
ufyekaji miti. Ili kuhakikisha hifadhi hiyo inalindwa, Serikali imeweka kambi
maalum ya ulinzi katika eneo la Gongoki, ambapo askari wa TFS wameimarisha
doria za mara kwa mara.
Katika ziara hiyo, CP Wakulyamba ametembelea vituo vikuu
vitatu vya kijiji cha Bondo vilivyokuwa na makazi kabla ya utekelezaji wa hatua
za uhifadhi, ambavyo ni Chelekachakomba, Doro Centre, na Gongoki.
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea
kutekeleza mikakati madhubuti ya uhifadhi, ikiwa ni pamoja na:
• Kuimarisha doria na udhibiti wa
uvamizi wa misitu kwa kutumia askari wa TFS na vyombo vya usalama.
• Uwekaji wa alama na mabango ya
mipaka ili kuzuia uingizwaji holela wa watu katika hifadhi.
• Kuhamasisha jamii zinazozunguka
hifadhi kushiriki katika kulinda rasilimali za misitu kupitia programu za elimu
ya uhifadhi.
Juhudi hizi ni sehemu ya utekelezaji wa sera za uhifadhi wa
mazingira na misitu ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na
upotevu wa bioanuwai.




0 Maoni