Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameitaka jamii kuongeza nguvu ya kumpa fursa ya elimu mtoto wa kike kuanzia ngazi ya familia ikiwa ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii.
Dkt. Biteko amesema hayo jijini Dar es Salaam katika
Kongamano lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communication “citizen rising
woman” ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani machi 8,
2025.
“tuanze nalo katika ngazi ya familia kwa kuwa ndiyo msingi
wa maendeleo katika jamii. Maendeleo ya jamii yeyote ile huanzia katika ngazi
ya familia. Hivyo, sisi tumwendeleze mwanamke kwa kumpatia na kumfungulia fursa
mbalimbali za elimu,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika maeneo kadhaa
ikiwemo kuwawezesha wanawake kujikomboa dhidi ya umaskini, kuboresha
upatikanaji wa huduma za afya, kushiriki katika nafasi mbalimbali za maamuzi na
hivyo kupiga hatua katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“wakati tunaposherehekea siku ya wanawake duniani, ni muhimu
pia kusherehekea mafanikio tuliyopata katika kutatua changamoto za haki za
wanawake hasa katika vipengele 12 vya Mwongozo wa mkutano wa Beijing,” amesema Dkt.
Biteko.
Aidha, amesema wakati Duniani inaasherehekea siku ya
wanaweke kimataifa, kuna ulazima wa kutambua na kuzifanyia kazi changamoto
zilizopo huku akizitaja baadhi yake kuwa ni ukatili wa kijinsia hasa maeneo ya
vijijini, mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwa wananchi na uelewa mdogo
kuhusu masuala ya kijinsia hasa katika maeneo ya vijijini.
“Naomba niwakumbushe na maneno ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kutokea katika Taifa hili aliyoyasema mwaka jana katika hafla kama hii. Nanukuu “Ningependa kuona usawa wa kijinsia wa 50/50, lakini si kwa ajili ya takwimu tu, bali kuhakikisha wanawake tunasonga mbele, tukiwa na uwezo wa kuleta mabadiliko,” mwisho wa kunukuu.
Pia amewahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika
mchakato wa uchaguzi na kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika baadaye mwaka huu ambapo amesema ni muhimu kuona wanawake
wakishiriki sio tu kama wapiga kura, bali kama wagombea, watetezi wa haki, na
viongozi wa mabadiliko.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi amehimiza utamaduni wa kusoma vitabu
vinavyoeleza umuhimu wa kumkomboa mwanamke kwa malengo ya kuikomboa jamii dhidi
ya misingi ya ubaguzi.
Akinukuu kitabu kilichoandikwa na Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zaidi ya miaka 80 iliyopita, Profesa Kabudi
amesema mapambano dhidi ya ubaguzi wa kijinsi yameanza miaka mingi iliyopita na
lengo lilikuwa ni kumkomboa mwanamke na kumwezesha kushika Madaraka na
kushiriki nafasi za uongozi.
“Malengo ya Mwalimu Nyerere bila shaka yametekelezeka kwa
kuwapata wanaweke viongozi na mfano halisi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Profesa
Kabudi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert
Chalamila amesema umefika wakati wa kurejea na kuondokana na mila mbaya
zinazosababisha ukatili wa kijinsia.
Awali, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communication, Victor Mushi aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuunga mkono jitihada za kukuza vipaji na kuwaibua wanawake wenye mafanikio ikiwa ni njia mojawapo ya kuiwezesha jamii kuondokana na ukatili.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni