WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema vijana wenye elimu na
maarifa ya dini ni nguzo muhimu ya ustawi na maendeleo katika jamii kwani imani
imara ya kidini hujenga jamii zenye maadili mema, ufanisi katika kazi, na
upendo wa dhati kwa kila mmoja.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ina matarajio
makubwa kwa vijana wanaoshiriki mashindano Quran kwani kwa kutumia maarifa na
ujuzi wanaoupata katika mashindano hayo kutekeleza majukumu muhimu ya kijamii
na kiroho.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Machi 8, 2025)
alipozungumza na wananchi katika Mashindano ya 16 ya Kuhifadhi Quran Tukufu
ngazi ya Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika katika uwanja wa Azam Complex
Chamanzi, Dar es Salaam.
“Mashindano haya ni fursa ya kukuza imani na maarifa yenu.
Kuhifadhi Quran ni jambo lenye manufaa mengi kwani inaimarisha uhusiano wenu na
Mwenyezi Mungu na inajenga msimamo wa kiroho. Nina hakika mnapokuwa na imani
imara, nidhamu, na maadili mazuri baadaye mtakuwa viongozi bora wa familia,
jamii, na Taifa kwa ujumla.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa mashindano hayo yana mchango mkubwa
katika kuimarisha amani, mshikamano na utulivu wa nchi, pia yanachangia katika
kukuza sekta mbalimbali ikiwemo ya uchumi na utalii kwani kila mwaka washiriki
kutoka mataifa mbalimbali wanakuja nchini kushiriki au kushuhudia mshindano
hayo.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa mashindano ya kuhifadhi
Quran, Waziri Mkuu amesema mashindano hayo yana manufaa kwa washiriki na kwa
Taifa kwani yanawawezesha washiriki kuwa na uwezo wa kuhifadhi na kuelewa
mafundisho ya Quran Tukufu. “Kupitia mashindano haya, tunawahamasisha vijana
wetu kuwa na moyo wa kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa juhudi kubwa.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuipongeza
taasisi ya Mana'Hil AL - Irfan kwa juhudi zao kubwa katika kuandaa mashindano
hayo. “Uwezo wa kuwa na mashindano haya kwa miaka 16 mfululizo ni dalili ya
dhamira thabiti ya kuwahamasisha vijana wetu katika kuzingatia na kuhifadhi
Quran Tukufu na kuhakikisha kwamba tunalinda utamaduni wa dini, maadili na
imani ya Kiislamu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali inaunga mkono
taasisi zote zinazojitahidi kuinua elimu ya dini na maadili, kwa lengo la kuwa
na Taifa lenye vijana bora, wenye imani thabiti na maadili mema.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa viongozi dini waendelee kuliweka suala la kudhibiti mmomonyoko wa maadili kuwa ajenda ya kudumu katika vikao na mikutano yao.“Ninawasihi sana endeleeni kukemea vikali vitendo vyote ambavyo vinamchukiza Mwenyezi Mungu na ni kinyume na maadili ya dini na utamaduni wa Mtanzania.”
0 Maoni