Wanawake kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
(TANAPA) wamejitokeza kushiriki katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani, ambayo Kitaifa yanafanyika leo Machi 8, 2025 katika viwanja
vya Sheikh Amri Abeid vilivyoko jijini Arusha ambapo Mgeni Rasmi katika
maadhimisho hayo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan.
Maadhimisho hayo yamelenga kutambua na kuenzi mchango wa
wanawake katika nyanja mbalimbali kwenye jamii, ikiwemo sekta ya uhifadhi na
utalii, ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa maendeleo ya Taifa letu.
Katika tukio hili la kihistoria, wanawake kutoka Shirika la
Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wameungana na wanawake kutoka maeneo mengine
nchini kusherehekea siku hii muhimu kwa kutoa elimu ya uhifadhi na utalii kwa
jamii ili kujenga jamii yenye uelewa mpana kuhusu masuala ya uhifadhi wa
rasilimali za Taifa.
Aidha, ushiriki wa wanawake kutoka TANAPA umelenga pia kuonesha juhudi zao katika kusimamia, kulinda na kutunza rasilimali za Taifa ambazo zimekuwa na matokeo chanya kiuchumi na kijamii, pamoja na kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu nafasi ya mwanamke katika sekta ya uhifadhi na utalii.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025.
0 Maoni