Mheshimiwa Macocha M. Tembele, Balozi wa Tanzania nchini
Indonesia amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Wataalamu kutoka Wizara
ya Fedha na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) uliopo
ziarani nchini Indonesia. Mazungumzo hayo yamefanyika mapema leo katika Ofisi
za Ubalozi wa Tanzania- Jakarta.
Katika mazungumzo yake, Mheshimiwa Balozi aliueleza ujumbe
huo kuhusu hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na Indonesia katika sekta ya
mafuta na gesi na kuwataka kutumia vyema fursa ya ziara hiyo ili kupata uzoefu
utakaoinufaisha Tanzania katika eneo la udhibiti na usimamizi wa shughuli za
mkondo wa juu katika utafutaji, uendelezaji na uzalishashaji wa mafuta na gesi.
Kwa upande wake Dr. Remidius Ruhinduka, Kamishna Msaidizi wa
Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha alimshukuru Mheshimiwa Balozi kwa
uratibu wa ziara pamoja na mapokezi mazuri waliyopata na kuahidi kuyafanyia
kazi maelekezo yake ipasavyo.
Ujumbe huo upo ziarani nchini Indonesia kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu zaidi utakaowezesha kufanikisha uandaaji wa kanzidata ya msingi wa bei na gharama za uendeshaji wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli Tanzania ambayo itaisasaidia nchi yetu kwenye majadiliano ya mikataba ya ugawanyaji wa mapato (PSA).



0 Maoni