WATUMISHI wa
Wizara ya Madini na Taasisi zake wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na uzalendo
ili kulinda uchumi wa nchi usiweze kuathirika na mabadiliko ya sera za mataifa
ya nje.
Akizungumza
leo Februari 8, 2025 katika Bonaza lililoandaliwa na Tume ya Madini na Shirika
la Madini la Taifa (STAMICO), lililofanyika katika Viwanja vya Shule ya
Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt.
Steven Kiruswa amesema Tanzania ina kila aina ya rasilimali ni vyema kuzitunza,
kuzithamini na kutanguliza uzalendo mbele ili uchumi wa nchi uendelee kuwa
imara.
“Nchi za
Falme za Kiarabu wametajirika kwa rasilimali moja tu ya uchimbaji mafuta, sisi
tuna kila kitu, madini ambayo tumepewa dhamana kubwa ya kusimamia tufanye kazi
kubwa kama timu kwa ushirikiano,” amesema Naibu Waziri Kiruswa.
Amesema, ili
kufikia lengo la asilimia 10 ambalo Sekta ya Madini inapaswa kuchangia katika
Pato la Taifa ni lazima kufunga mkanda.
“Tunapaswa
kufunga mkanda ili kufikia lengo la asilimia 10, siku zilizobaki si nyingi
ingawa tumepiga hatua kiasi kikubwa,”amesema, Mhe. Dkt. Kiruswa.
Awali
akizungumza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka
watumishi kuendelea kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii na kujituma, ili
Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa katika taifa na kuleta unafuu kwa
wananchi.
Naye
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo amewasihi watumishi katika Sekta
ya Madini kutunza afya kwa kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyo ya
kuambukiza.
Aidha,
Lekashingo amekabidhi tuzo maalum kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi
Ramadhani Lwamo kutokana na utendaji wake uliotukuka, busara zake na ukarimu
wake na kuaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye Januari 15, 2025
alimthibitisha rasmi kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini.
Wakati huohuo
Naibu Waziri Kiruswa ametoa tuzo na
zawadi mbali mbali kwa viongozi wastaafu ikiwa ni pamoja na kuwaaga rasmi
aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula na Profesa Abdulkarim Mruma aliyekuwa Kamishna wa Tume ya
Madini.
Katika hatua
nyingine washindi wa michezo mbalimbali wamekabidhiwa vikombe na medani.
Taasisi
zilizo chini ya Wizara ya Madini ni Tume
ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti
wa Madini Tanzania (GST), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji
katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI).
0 Maoni