Waziri wa
Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema, ujenzi wa Viwanda vinne vya Uchenjuaji
Madini ya Shaba ikiwemo kiwanda cha Shengde Precious Metal Resources Co.
Limited kinachoendelea kujengwa katika eneo la Mahungu Kata ya Nala Jijini
Dodoma vinatarajiwa kuwa mkombozi wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Shaba
nchini.
Waziri
Mavunde amebainisha hayo leo Februari 16, 2025 baada ya kutembelea na kukagua
maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho na kutoa pongezi kwa Kampuni ya Shengde
Precious Metal Resources Co. Limited kwa uwamuzi wa kujenga kiwanda hicho
Jijini Dodoma.
Aidha, Waziri
Mavunde amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu Mheshimiwa
Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuyaongezea thamani madini hapa
hapa nchini ili kukuza ajira kwa watanzania na kuongeza Pato la Taifa ambapo
amewaahidi kupatiwa ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini.
Pamoja na
mambo mengine, Waziri wa Mavunde amewataka Wamiliki wa kiwanda hicho
kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati ili kiweze kuanza uzalishaji kwa
lengo la kuongeza tija katika Sekta ya Madini ikiwemo kuongeza ajira kwa
watanzania, kipato kwa Wamiliki na kuongeza Pato la Taifa kupitia tozo mbalimbali.
Pia, Waziri
Mavunde amesema, kwa kipindi kirefu wachimbaji wa Madini ya Shaba wamekuwa
wakisafirisha Madini yao kwenda kuuza umbali mrefu ambapo viwanda vinapatikana
huku miundombinu ya usafirishaji malighafi hizo ikiwa na changamopo hivyo,
viwanda hivyo vitakuwa suluhisho la changamoto za usafirishaji na masoko kwa
wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini hayo.
Pia, Waziri
Mavunde amesema kwamba ujenzi wa viwanda kuongeza thamani madini ya shaba na
nikeli unaendelea maeneo mengi nchini ikiwemo Lindi na Chunya, Mbeya na kutoa
rai kwa mikoa kutenga maeneo maalum ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani
Madini.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule amesema Mkoa wa
Dodoma umebarikiwa kuwa na Madini ya aina mbalimbali ambao unaongoza kwa uwepo
wa aina nyingi za madini kuliko Mkoa wowote Tanzania na kuahidi kutenga eneo
kubwa kwa ajili ya viwanda vya uongezaji thamani madini ili kuifanya Dodoma
kuwa kitovu cha uongezaji thamani madini nchini.
Aidha,
Senyamule amempongeza Waziri Mavunde kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini
ambapo amesema Mkoa huo una vipaumbele vitano ikiwa Madini ni moja ya
kipaumbele cha Mkoa huo.
Awali, Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Bw. Msafiri Mbibo alianza kwa kuipongeza Kampuni
hiyo kwa uwamuzi wa kujenga kiwanda hicho Jijini Dodoma na kuahidi kutoa
ushirikiano kwa mwekezaji ili kufanikisha azma ya uongezaji thamani madini.
Naye,
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Bw. Abia Mafie ameiomba Wizara ya Madini
kupatiwa maeneo yenye taarifa za uwepo wa madini ya Shaba kwa wingi ili kupata
malighafi za kutosha katika uendeshaji wa kiwanda hicho ingawa watanunua
malighafi nyingi kutoka kwa wachimbaji wadogo.
Aidha, Mafie
amesema, pamoja na juhudi za Serikali kuwezesha uongezaji thamani madini
ufanyike hapa hapa nchini lakini bado kuna changamato ya usafirishaji wa
malighafi kutoka migodini mpaka kiwandani na ameiomba kuondolewa kwa baadhi ya
tozo katika uchenjuaji wa madini ya Shaba.
Pamoja na
mambo mengine, Mafie amesema mpaka sasa ujenzi wa Kiwanda hicho umegharimu
zaidi ya bilioni 3 ambapo kiwanda kinatarajiwa kuanza uzalishaji mapema ifikapo
Juni, 2025.
#Madinini
Ajira,Uchumi na Maendeleo
#InvestinTanzania Mining Sector




0 Maoni