Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali ya Tanzania
imejidhatiti kuboresha na kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuja na mipango kadhaa
yenye lengo la kuongeza fursa kwa wakulima nchini.
Dkt. Biteko
amesema hayo jijini New Delhi, India
wakati akishiriki mkutano kuhusu masuala ya mazao jamii ya mikunde.
“Tunaongeza
uwekezaji katika utafiti na kuboresha upatikanaji wa teknolojia za kisasa za
kilimo ambapo kila afisa wa ugani nchini amepewa vifaa vyote muhimu ikiwemo
pikipiki na kompyuta ili kutoa huduma nzuri na kwa wakati kwa wakulima wetu,” amesema
Dkt. Biteko.
Amesema
Serikali pia imeboresha shughuli za usafirishaji wa bidhaa ikiwa ni pamoja na
kurahisisha michakato ya uuzaji mazao "Tanzania inaendeleza ujenzi wa reli
ya kisasa (SGR) ambayo itaimarisha usafirishaji wa bidhaa yenye urefu wa
takribani kilomita 500 kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo
imekamilika na na inatumika.
Vilevile,
amesema kupitia mradi wa BBT (Building a Better Tomorrow) Serikali imewezesha
vijana kwa kuwapa ardhi, fedha na upatikanaji wa masoko sambamba na kuongeza
huduma za kifedha za kidijitali.
Aidha, Dkt.
Biteko amesema “India ni soko muhimu kwa mazao jamii ya kunde kutoka Tanzania
na tunaweza kupata mafanikio makubwa zaidi. Leo nawaalika wawekezaji kutoka
India na nchi nyingine duniani kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo ya Tanzania
kuanzia uzalishaji wa kisasa wa soya hadi uwekezaji katika mifumo ya usimamizi
wa mavuno.”
Akizungumzia
maendeleo ya sekta mazao jamii ya mikunde, amesema kuwa mwaka 2023, Tanzania
ilizalisha takriban tani 250,000 za mbaazi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 56
ikilinganishwa na mwaka 2018.
Inakadiriwa
ifikapo mwaka 2030 Tanzania itakuwa na ukuaji mkubwa katika Pato la Taifa
kupitia Kilimo, ambapo mauzo ya maharage mekundu, mbaazi na choroko
yanatarajiwa kufikia dola bilioni 1.47, dola milioni 84 na dola milioni 115.
Aidha, ili kufikia uwezo huo, Tanzania imeweka mikakati ya kukuza sekta ya
mazao jamii ya kunde kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa wakulima
kusajiliwa, kuboresha mbinu za kilimo na teknolojia, kuhakikisha ubora na
viwango vya mazao kulingana na mahitaji ya soko.
Pamoja na hayo
Dkt. Biteko amesema “Mazao jamii ya kunde nchini Tanzania yanauzwa kupitia
mnada wa mtandaoni ambao unatoa fursa kwa wafanyabiashara kupata taarifa kuhusu
mizigo iliyohifadhiwa katika ghala lililosajiliwa.”
Amesisitiza
“Mfumo huu unahakikisha uwazi, ufuatiliaji na ufanisi katika biashara ya
kimataifa. Mwaka 2024 pekee kupitia mfumo huu, wakulima wa Tanzania walipata
zaidi ya dola milioni 91.31 kutoka katika biashara ya mbaazi, dengu na
maharagwe ya soya, ubunifu huu si tu unaimarisha ushindani wetu bali pia unafungua
fursa mpya za ushirikiano.”
Kufuatia hali
hiyo,kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kimeongezeka na kufikia dola
bilioni 7.9 kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Pia, mwaka 2023 mauzo ya mbaazi
kutoka Tanzania kwenda India yalifikia tani 186,447 yenye thamani ya dola
milioni 139.1.
0 Maoni