Njombe
imeendelea kufanya vizuri katika sekta ya elimu kwa mwaka 2024/2025, ikiwa
miongoni mwa mikoa iliyopata mafanikio makubwa katika matokeo ya mitihani ya
upimaji wa Darasa la Nne na ule wa kumaliza Darasa la Saba. Haya yamebainishwa
katika kikao cha tathmini ya matokeo hayo, ambacho kimewakutanisha walimu wakuu
wa shule za msingi na maafisa elimu wa mkoa, kwa lengo la kujadili mbinu za
kuimarisha ufaulu zaidi kwa mwaka 2025/2026.
Akizungumza
katika hafla ya utoaji wa vitabu vya ziada kwa shule za msingi na sekondari,
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amepongeza juhudi za walimu na
maafisa elimu katika kuinua viwango vya ufaulu mkoani humo. Amesema mafanikio
haya ni ishara ya mshikamano baina ya serikali, walimu, wazazi na wadau wa
elimu.
“Hatuwezi
kuficha mafanikio haya-Njombe inazidi kung’ara katika sekta ya elimu.
Tunashuhudia ongezeko la ufaulu kwa kasi nzuri, jambo linaloonyesha kuwa juhudi
zetu za kuwekeza katika elimu zina matokeo chanya. Nawapongeza walimu na
maafisa elimu kwa kazi kubwa wanayoifanya,” alisema Mhe. Mtaka.
Katika hafla
hiyo, Mhe. Mtaka pia alipokea vitabu vya ziada vilivyotolewa na mdau wa elimu,
Africa Proper Education Network, kama zawadi kwa jitihada zake za kuimarisha
sekta ya elimu mkoani Njombe. Alimpongeza mdau huyo kwa kuona umuhimu wa
kushirikiana na serikali katika kuinua ubora wa elimu.
“Elimu ni
msingi wa maendeleo yetu, na tunapopata wadau wanaojitoa kwa dhati kama Africa
Proper Education Network, ni faraja kubwa. Hii ni ishara kwamba elimu si jukumu
la serikali peke yake, bali ni wajibu wa jamii nzima,” aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe.
Mtaka ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa za kuboresha
miundombinu ya elimu nchini, ikiwemo ujenzi wa shule mpya, madarasa, mabweni na
uwezeshaji wa walimu.
“Serikali ya
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza na kuboresha kwa kiwango kikubwa
miundombinu ya elimu, hali inayowapa wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia na
walimu mazingira mazuri ya kufundishia. Haya ni mafanikio makubwa tunayopaswa
kuyathamini na kuyatumia kikamilifu ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu
bora,” alisisitiza Mhe. Mtaka.
Katika kikao
hicho, walimu na maafisa elimu walikubaliana kuongeza juhudi zaidi ili
kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi unaendelea kuimarika kwa mwaka 2025/2026, huku
ushirikiano wa wadau wa elimu ukiendelea kupewa kipaumbele.
0 Maoni