Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kuwabana wamiliki wote wa ardhi
wasiolipa kodi ya pango la ardhi sambamba na kutoendeleza maeneo wanayomiliki.
Wakiwa katika
ziara ya kukagua utekelezaji wa sharti la kulipa kodi na kuendeleza kwa
wamiliki wa ardhi Mkoa wa Pwani tarehe
13 februari 2025, timu maalum ya ukaguzi kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na
Mandeleo ya Makazi imesema hatua hiyo ni juhudi za wizara kukusanya kodi pamoja
na kuhakikisha maeneo yanayomilikiwa na
wananchi yanaendelezwa.
Kamishna wa
Ardhi Msaidizi Mapato na Uwekezaji Wizara ya Ardhi Bw. Leonard Msafiri amesema,
kwa mujibu wa sheria wamiliki wa ardhi wanatakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi
na wasipofanya hivyo wanapaswa kupewa notisi ya kulipa ndani ya siku kumi na
nne.
‘’Ulipaji wa
kodi ya ardhi ni wajibu wa kisheria kwa mmiliki chini ya fungu 33 la sheria ya
ardhi sura 113,’’amesema.
Akiwa katika
shamba namba 57, 58, 59 na 60 lilipo Miswe Kibaha Mkoani Pwani, Kamishna wa
Ardhi Msaidiźi Mapato na Uwekezaji Wizara ya Ardhi amemweleza mmiliki wa
mashamba hayo kuwa ana nafasi ndani ya siku kumi na nne kulipa kodi ya ardhi.
Aidha, Kamishna
wa ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani Ndg. Hussein Sadiki Iddi, ameeleza kuwa ndani
ya siku hizo kumi na nne mmiliki anaweza kufika Ofisi za ardhi ili kupewa
ushauri na kueweka namna nzuri ya kufanya mazungumzo ya kulipa deni
linalomkabili.
Timu ya ukaguzi
ilitembelea pia shamba namba 2 eneo la Miswe kata Mbwawa, halmashauri ya
manispaa Kibaha ambapo mmiliki wake anadaiwa kiasi cha Tsh mil 690. Katika eneo
hilo Kamishna Msafiri alielekeza mmiliki wake kupatiwa barua ya onyo ikiwa ni
hatua ya kwanza ya mchakato wa ufutaji ardhi kwa mujibu wa fungu la 45 ya
sheria ya ardhi sura ya 113. Barua hiyo alikabidhiwa Bw. Dunia Mrisho Kinyogoli
ambaye ni mwakilishi Miswe
Vile vile,
timu hiyo ilitembelea kituo cha mafuta cha ATN picha ya ndege mkoani Pwani ambapo
mmiliki wake amadaiwa kiasi cha Tsh 24. Mmiliki huyo alikabidhiwa barua ya onyo
kupitia Meneja wa kituo Bw. Abdallah Bawazir.
Kamishna
Msafiri alieleza kuwa zoezi la kufuatilia madeni ya kodi ya pango la ardhi ni
endelevu na linafanyika katika mikoa yote hivyo amehimiza wadaiwa wote wa kodi
ya pango la ardhi kuhakikisha wanalipa madeni yao ili kuepuka usumbufu unaoweza
kuwapata wakati wa kuendesha shughuli zao.
0 Maoni