Oparesheni maalumu ya kuwadhibiti wanyamapori wakali na
waharibifu aina ya fisi waliokuwa wanaleta taharuki na madhara Kwa jamii
inayoendelea Mkoani Simiyu imeonesha mafanikio makubwa baada ya fisi 16 kuvunwa
ikiwa ni hatua muhimu iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na
Utalii ya kuhakikisha usalama na utulivu Kwa wananchi vinarejea.
Hayo yamesemwa leo Februari 19, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu Mhe. Kenani Kihongosi alipokuwa akiongea na waandishi wa vyombo
mbalimbali vya habari.
Mhe. Kihongosi amesema kufuatia changamoto hiyo, Serikali ilichukua jukumu kubwa la
kuhakikisha inalinda wananchi wake ikiwemo kuanzisha oparesheni maalumu
inayohusisha Jeshi la Uhifadhi Kwa Taasisi za TAWA, TANAPA na TFS Kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi, oparesheni inayotajwa
kuanza Januari 25, 2025.
"Tarehe 20/12/2024 baada ya fisi kuvamia wananchi
Serikali ilichukua hatua kubwa ya kushirikisha vyombo vyake (TAWA na Jeshi la
Polisi) na kuanza Oparesheni, lakini ilipofika tarehe 25/01/2025 oparesheni ya
mkoa mzima ilifanyika Kwa ukubwa kuhakikisha inakabiliana na fisi wote
waliokuwa wanasumbua wananchi," amesema Mhe. Kihongosi.
"Na Kwa taarifa njema ni kwamba tangu kuanza Kwa
oparesheni hii vyombo vyetu vimeweza kudhibiti na kuua fisi 16 na ndio maana
kwasasa mnaweza kuona hali imetulia," ameongeza Mkuu huyo wa mkoa wa
Simiyu.
Aidha, Mhe. Kihongosi ameendelea kuwatoa hofu wananchi wa
mkoa huo akisisitiza kuwa hali ni shwari na kuwataka waendelee na shughuli zao
kama kawaida huku akikemea vikali imani za kishirikina kuhusiana na mnyamapori
aina ya fisi kwa baadhi ya wakazi wa Simiyu na kuwataka wote wanaofuga
wanyamapori pori hao kuacha mara moja kwani ni kosa kisheria kumiliki nyara za
Serikali bila Kibali.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja
amewaomba wananchi wa Mkoa wa Simiyu hususani wilaya ya Itilima kuacha tabia ya
kutembea nyakati za usiku na alfajiri kwani ni nyakati ambazo wanyama fisi huwa
katika mawindo yao.
Vilevile amewasisitiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano
kwa Maofisa wa Jeshi la Uhifadhi waliopo uwandani ili kuongeza ufanisi wa zoezi
hilo huku akiwahakikishia kuwa Serikali
imedhamiria kulinda wananchi wake na kwamba Askari wapo uwandani wanafanya Kazi
usiku na mchana kuwahakikishia usalama wao.
Kwa upande wao wananchi wa Simiyu hususani wilaya ya Itilima
wameshukuru Kwa juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na
changamoto hiyo, wakisema kuwa hatua hiyo imeweza kuwarejeshea matumaini,
utulivu na amani.
"Kwakweli tulikuwa tunasumbuliwa sana na haya mafisi ambayo yalikuwa yanauma watu, baada ya Serikali kusikia ikaweka ulinzi, kwakweli imetufanyia vizuri sana mpaka leo hatujawasikia tena tangu Askari waanze kuwashambulia hao fisi, mpaka leo hii tuna utulivu sana kwakweli tunashukuru sana," amesema Mozo Mabula mkazi wa Kijiji cha Mwamunhu kilichopo wilaya ya Itilima.
0 Maoni