Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto
Biteko ameagiza Mwanafunzi Mirabelle Msukari na Wenzake wa Shule ya Msingi Sun
Rise iliyopo Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam kupelekwa katika Mradi wa
kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili kujifunza zaidi kwa Vitendo namna
mradi huo unavyozalisha Umeme.
Mheshimiwa Biteko amesema
hayo leo Februari 18 kwa njia ya simu baada ya Naibu Waziri wa Nishati
Mheshimiwa Judith Kapinga kutembelea
shule hiyo kwa lengo la kumpongeza mwanafunzi huyo ambaye video yake ilijizolea
umaarufu kupitia mitandao ya kijamii ambapo
Mirabelle alielezea kwa ufanisi juu ya miradi mbalimbali ya umeme
inayotekelezwa nchini ukiwemo mradi wa Julius Nyerere.
“Sisi tukupongeze na tumefurahi kwa umri wako unafuatilia masuala
ya Nishati, sasa tutakupeleka kuliona Bwawa la Julius Nyerere uone Umeme
unavyozalishwa ili uendelee kujifunza zaidi. Sisi tunatamani kukuona
ukifanikiwa zaidi,” amesema Mhe. Biteko.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Judith
Kapinga amesema Miradi hii ya kimkakati ambayo inatekelezwa nchini ni jitihada
za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dokta
Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha dhamira ya dhati kuendeleza miradi ya umeme nchini ukiwemo
mradi wa JNHPP ambao kwa sasa umefikia asilimia 99.8.
“Wakati Mheshimiwa Rais anaingia madarakani, Mradi wa Julius
Nyerere ulikuwa asilimia 33, leo tunavyozungumza umefikia zaidi ya asilimia 99
na mashine nane tayari zimeingizwa kwenye gridi ya Taifa. Imebaki mashine moja
pekee ambapo mradi uko mbioni kukamilika,” amesisitiza mheshimiwa Kapinga.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa wateja
Bi. Irene Gowelle akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO), amesema wamepokea kwa vitendo agizo la Mheshimiwa
Dkt. Biteko la kuhakikisha mwanafunzi huyo anafanya ziara katika Mradi wa
Julius Nyerere ambapo pia amefafanua kuwa elimu na taarifa zinazotolewa na
TANESCO zinawafikia walengwa kwa usahihi.
“Hatua hii inatupa nafasi ya kuona kwamba elimu na taarifa
mbalimbali tunazozitoa zinawafikia moja kwa moja makundi mbalimbali i? wakiwemo watoto na ndio maana mmeweza kuona Mirabelle
akizungumza kwa ufasaha.
Sisi kama Shirika la Umeme tutaendelea kufanya hivyo,”
amefafanua Bi. Gowele.
Mwanafunzi huyo licha ya pongezi, amepewa zawadi mbalimbali ikiwemo Komputa Mpakato (Laptop) pamoja na fedha kiasi cha Shilingi Milioni Mbili.
0 Maoni