Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane jana Februari 15 ilipokea takribani watalii 109 katika kilele cha Kampeni ya “Valentine Weekend Gateaway na TANAPA” iliyozinduliwa Januari 24, 2025 iliyolenga kuhamasisha watalii kutembelea Hifadhi za Taifa Tanzania katika msimu wa Sikukuu ya wapendanao.
Watalii hao
109 iliwahusisha watalii wa ndani 98 na wengine 11 wakitoka nje ya mipaka ya
Tanzania, wageni hao waliofika katika majira tofauti ambapo asubuhi waliingia
watalii 60 na alasili walifika 49 miongoni mwao walilala katika mahema. Licha
ya kutembelea vivutio mbalimbali nyakati za mchana pia walipata fursa ya
kufurahia utalii wa usiku ikiwemo kuota moto usiku, safari za boti za usiku
pamoja na utalii wa kuangalia nyota.
Akiwakaribisha
Watalii hao Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk. Tutindaga George, Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, aliwapongeza watalii hao kwa kuchagua
kutembelea Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane wakati wa mchana na usiku, kwani
nyakati za usiku jiji la Mwanza linamuoneka mzuri na kitofauti.
Aidha,
Kamishna Dk. Tutindaga alisema, “Tunayo furaha kuwapokea leo hii, mmetutoa
kimasomaso kwa kutembelea Hifadhi hii kwani mmehamasika vya kutosha na leo hii
tumeona matunda ya uhamasishaji tulioufanya katika vyombo mbalimbali vya
habari, ni matumaini yetu kama TANAPA kuwa mtafurahia urithi wenu na
mtakaporudi katika maeneo yenu ya kazi mtakuwa mabalozi kuitangaza hifadhi hii
na kuwaleta watanzania wengine nao waje wafurahie tunu hizi.”
Naye,
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Jully Lyimo, anayesimamia Kitengo cha Maendeleo
ya Biashara TANAPA Makao Makuu, alielezea kuwa Kampeni ya Valentine “Weekend
Gateaway na TANAPA” imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na watalii wengi
kutembelea Hifadhi za Taifa, aidha kwa watalii waliotembelea Saanane
wamefurahia utalii wa boti usiku “Night Boat Excursion”. Utalii huu wa boti
usiku unakupa mwonekano na radha tofauti na utalii wa mchana kwani mandhari
nzuri ya jiji la Mwanza na mwangaza wa stima ulioakisiwa na maji ya Ziwa
victoria inakupa taswira isiyosahaulika maishani.”
Kamishna
Jully aliongeza, “Wageni wamefurahi sana kutalii na boti usiku, kula chakula na
vinywaji kwenye boti, kucheza muziki pamoja na kulala kwenye mahema ndani ya
Hifadhi. Tunashukuru kwa huu muitikio uliopo na tunaamini aina hii ya utalii wa
matukio utaendelea kukua na watanzania kuhamasika kuembelea Hifadhi za Taifa
Tanzania.
TANAPA
imeendelea kunadi na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za
Taifa nchini hasa kupitia matukio ambayo yanachangia hamasa ya watanzania
kutembelea Hifadhi za Taifa na kupelekea ongezeko la pato la Taifa pamoja
na kukuza uchumi.





0 Maoni