FCC yampongeza Rais Samia kufanikisha maboresho ya sheria ya ushindani

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Bw. William Erio amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha Marekebisho ya Sheria ya Ushindani ambayo yalikuwa yamekwama kwa karibu miaka 10.

Bw. Erio ametoa pongezi hizo leo Jijini Dar es Salama katika kikao kazi kati ya Tume ya Ushindani na Wahariri wa Vyombo vya Habari, ambapo pia ameishukuru Serikali pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukamilisha maboresho hayo.

“Katika hili napenda kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kukamilisha maboresho ya sheria ya ushindani ndani ya mwaka mmoja, ambayo hapo awali yalikuwa yamekwama kwa karibu miaka 10,” amesema Bw. Erio.

Aidha, Bw. Erio amesema Tume ya Ushindani imefanikiwa kupata cheti cha Ithibati cha Utoaji Huduma cha Kimataifa (ISO), “wateja wetu wote sasa wajiandae kupata huduma bora kutoka kwa kwetu FCC.”

Akiongelea tatizo la bidhaa Bandia Mkurugenzi wa Kudhibiti Bidhaa Bi. Khadija Juma Ngasongwa amesema bado lipo nchini kwa bidhaa karibia zote, zikiwamo za umeme, vitambaa, vifaa vya ujenzi, vipuri vya magari, dawa pamoja na vinywaji.

“Takwimu za kimataifa za Interpol zinaeleza kuwa bidhaa bandia ni biashara kubwa zaidi kuliko hata ya ile ya dawa za kulevya.. na vita yake ni ngumu kuliko ya dawa za kulevya,” amesema Bi. Khadija.

Kuhusu madai ya kuwapo kwa vinywaji vinavyodaiwa kusababisha Saratani, Bi. Khadija amesema kwamba Tume ya Ushindani kwa kushirikiana na Shirika la Viwango nchini linafanya uchunguzi ili kubaini ukweli.





Chapisha Maoni

0 Maoni